Na. Majid Abdulkarim
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Wataalamu Tanzania na Osaka (TOA) kuwasilisha michango yao kwa wakati na kushiriki mikutano ya kikatiba ili kujenga uimara wa Jumuiya hiyo.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa kumi wa wanachama wa TOA.
“Uimara wa jumuia ni michango na vikao kwani TOA inaendeshwa kwa kutumia michango ya ada na viingilio vya wanachama pamoja na ruzuku kutoka Shirika la Maendeleo la Japani(JICA)” amesema Nyamuhanga.
Pia Nyamuhanga ameeleza kuwa kupitia mkutano huo wanachama watapata kubadilishana mawazo na uzoefu jinsi ya utekelezaji wa azma ya serikali katika kuwafikishia wananchi wake huduma nzuri na kwa ufanisi wa hali ya juu.
Nyamuhanga ameendelea kusisitiza kuwa wanachama hao waendelee kutumia jumuiya hiyo kuongeza chachu katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Naye Mwenyeki wa TOA Profesa Riziki Shemdoe awali akitoa taarfa fupi ya jumuiya hiyo amesema kuwa katika mkutano huo watajadili maboresho ya katiba ya TOA , mpango mkakati na suala kubwa la kubadilisha jina la jumuiya hiyo.
Akiendelea kusema Profesa Shemdoe amesema kuwa TOA inamadeni ambayo ni ya muda mrefu yanayofikia kiasi cha shilingi zaid ya milioni 4000, kitu ambacho kinafanya umoja huo kuwa tegemezi zaidi kuliko ambavyo tungeweza kujiendesha.
“Kutokana na changamoto hiyo uongozi unaendelea kuhamasisha wanachama kulipa michango yao lakini bado kuna kusuasua” ameeleza Profesa Shemdoe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Makatibu Tawala Mikoa ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Rehema S. Madenge akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake amesema kuwa kupitia mkutano huu watapata kufanya uhamasishaji kwa kutekeleza yote yaliyoelekezwa na viongozi wao.
TOA ilianzishwa rasmi kama Jumuiya ya Umoja wa Wataalam waliyopata mafunzo ya ugatuaji wa madaraka Jijini Osaka, Japani, baadaye katiba ya TOA iliboreshwa na uwanachama na kuwa Taasisi (Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa) pamoja na washiriki wa mafunzo ya Osaka- Japani.