Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa majukumu na upatikanaji wa fedha katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Uendelezaji wa Rasilimali ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) katika kipindi cha nusu mwaka wa 2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa majukumu na upatikanaji wa fedha katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Uendelezaji wa Rasilimali ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) katika kipindi cha nusu mwaka wa 2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, wakiwa katika kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Kikao hicho kililenga kutoa taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa majukumu na upatikanaji wa fedha katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Uendelezaji wa Rasilimali ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) katika kipindi cha nusu mwaka wa 2019/2020 kilichofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula akizungumza jambo katika kikao kati ya Kamati hiyo na Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilicholenga kupata taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa majukumu na upatikanaji wa fedha katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Uendelezaji wa Rasilimali ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) katika kipindi cha nusu mwaka wa 2019/2020. kushoto kwake ni Katibu wa Kamati hiyo, Felister Mgonja.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Rasilimali ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa majukumu na upatikanaji wa fedha katika kampuni hiyo katika kipindi cha nusu mwaka wa 2019/2020.
………………..
Na Teresia Mhagama, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kupitia Mwenyekiti wake, Dunstan Kitandula imewapongeza viongozi wa Wizara ya Nishati, kwa usimamizi wao unaoendelea kuboresha utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuhakikisha kuwa Shirika hilo linatekeleza majukumu yake ipasavyo na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 18 Januari, 2020 jijini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati hiyo na watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
Kikao hicho kilikuwa mahsusi kwa ajili ya utoaji wa taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa majukumu na upatikanaji wa fedha katika Shirika la Umeme Tanzania na Kampuni ya Uendelezaji wa Rasilimali ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) katika kipindi cha nusu mwaka wa 2019/2020.
“ Tunaona jitihada zinazofanyika za kuiboresha TANESCO na sisi tunakupongeza Waziri na timu yako, lakini bado kuna vitu vya kurekebisha ikiwemo kuwafanya baadhi ya watumishi wa TANESCO kutoka kwenye ufanyaji kazi wa kimazoea unaotokana na kuona kuwa Shirika hili ni la umma na wawe na mtazamo wa kibiashara ambao utaliletea faida Shirika huku likitoa huduma bora kwa wananchi.” Alisema Kitandula
Kitandula pia alisisitiza kuwa, kasi ya kuunganisha wananchi na huduma ya umeme iongezeke pamoja na uboreshaji wa utoaji wa taarifa kwa wananchi akitolea mfano kuwa, inapotokea changamoto ya umeme, wananchi wapewe taarifa ndani ya muda muafaka na kuwe na mawasiliano chanya kati ya mteja na watoa huduma wa TANESCO.
Aidha, Kamati ya Bunge iliipongeza TANESCO kwa kuacha kutegemea ruzuku kutoka serikalini ili kujiendesha na kwa mara ya kwanza imetoa gawio serikalini la shilingi bilioni 1.436 katika mwaka 2019.
Kuhusu TGDC, Kamati iliipongeza kampuni hiyo kwa jitihada zake za kuhakikisha kuwa Jotoardhi inaendelezwa na kusema kuwa kampuni hiyo ni muhimu katika uendelezaji wa rasilimali hiyo ambayo ni moja ya vyanzo vya nishati jadidifu nchini na itawezesha juhudi za Serikali za kuwa na umeme wa uhakika kwani Tanzania ina uwezo wa kuzalisha umeme wa Jotoardhi usiopungua megawati 5000.
Waziri wa Nishati, awali, alipata fursa ya kueleza hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme ambapo katika uzalishaji umeme alisema kuwa uwezo wa mitambo ya kufua umeme nchini umefikia jumla ya megawati 1,602.318 huku mahitaji ya juu katika mfumo wa gridi ya Taifa yakifikia megawati 1,120.12 ambayo yalifikiwa tarehe 27 Novemba, 2019.