Home Mchanganyiko DKT.KALEMANI AELEZA FAIDA NA MIKAKATI YA KUENDELEZA GESI ASILIA NCHINI

DKT.KALEMANI AELEZA FAIDA NA MIKAKATI YA KUENDELEZA GESI ASILIA NCHINI

0

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani(kwanza kulia) akisikiliza maoni mbalimbali kutoka kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na madini(hawapo pichani) mara baada ya kuwasilisha taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu utekelezaji wa hali ya upatikanaji wa fedha za maendeleo katika kampuni ya Taifa ya Mafuta(TPDC) kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kushoto kwake ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt.Adelardus Kilangi.

Wajumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa katika kikao na Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilicholenga kujadili kuhuku kuhusu utekelezaji wa hali ya upatikanaji wa fedha za maendeleo katika kampuni ya Taifa ya Mafuta(TPDC) kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

……………….

Hafsa Omar-Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amesema Ugunduzi wa Gesi Asilia nchini umepelekea kuimarika kwa uzalishaji wa umeme nchini ambapo kwa sasa asilimia 57.02 ya umeme unaozalishwa nchini unatokana na nishati hiyo.

Aliyasema hayo, Januari 17, 2020 wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini  kuhusu utekelezaji wa majukumu na hali ya upatikanaji wa fedha za maendeleo kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Aidha, alisema alisema kuwa tangu Gesi asilia ilivyoanza kutumika kama nishati mbadala kwa matumizi mbalimbali, tangu mwaka 2004  hadi Disemba 2019, Serikali imeokoa zaidi ya dola za Marekani 13.048 ambazo ni sawa shilingi trilioni 30.225.

Dkt. Kalemani pia alielezea maendeleo ya miradi mbalimbali ya utafutaji wa Mafuta na Gesi ambayo ni mradi wa kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini, kitalu cha Eyasi-wembere na  kitalu Namba 4/1B.

Kuhusu kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini alisema kuwa, mradi huo unalenga kufanya utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia katika Kitalu hicho kilichopo katika bahari ya kina kirefu kusini mwa Tanzania na kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na kukamilisha data za mitetemo za mfumo wa 3D na kukamilisha uchambuzi wa kiufundi wa zabuni ya kumpata mshauri mwelekezi wa uchorongaji wa visima vya utafiti.

Aliongeza kuwa kazi za uchorongaji katika Kitalu hicho utaanza inatarajiwa kuanza ifikapo mwezi Agosti, 2020 na kukamilika mwezi Oktoba, 2020.

Aidha, Mradi wa Eyasi-Wembere alisema kuwa, unalenga kufanya utafutaji wa mafuta na kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na kukamilisha uchorongaji wa visima viwili vifupi vya utafutaji katika maeneo ya Kining’inila- Igunga na Nyaranja-Meatu kwa ajili ya kuchukua sampuli za miamba na kutoa elimu kwa jamii kuhusu mradi huo.

Vilevile alisema kuwa, kazi ya kuchoronga kisima cha tatu katika eneo la Luono-Iramba itaendelea na kukamilika mwezi Februari 2020.

Dkt. Kalemani pia alitoa taarifa kuhusu mradi wa utafutaji Mafuta na Gesi katika Kitalu Namba 4/1B kilicho katika bahari ya kina kirefu kusini mwa Tanzania ambapo alisema kuwa kazi ya ukusanyaji wa data katika kitalu hicho itaanza mwezi Machi na kukamilika mwezi Juni 2020.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio  alisema kuwa, kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba mwaka jana,  Shirika hilo limekusanya zaidi ya shilingi bilioni 293 kutoka vyanzo vya ndani ikiwa ni sawa na asilimia 75 ya lengo la makusanyo ya nusu mwaka .

Aliongeza kuwa, mapato ya ndani yameongezeka kwa asilimia 6.4 yakilinganishwa na mapato ya shilingi bilioni 275.77 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2018/19.

Alisema, Shirika hilo linategemea vyanzo vya mapato ya ndani ambavyo ni pamoja na mauzo ya Gesi asilia, mapato yatokanayo na shughuli za mkondo wa juu, gawio la uwekezaji Songas na pamoja na vyanzo vingine.