*************************
NJOMBE
Naibu waziri wa afya maendeleo ya jamii ,jinsia wazee na watoto Dr Faustine Ndugulile ameutaja mkoa wa Njombe kuwa wa mfano wa kuigwa baada ya kufanikiwa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 250 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2005 hadi vifo 94 mwaka 2019 kiwango ambacho ni kidogo zaidi ikilinganishwa na cha taifa ambacho takribani vifo 556 hutokea kwa kila vizazi hai laki moja.
Licha ya kufanya vyema katika huduma za uzazi lakini takwimu za mwaka jana za mkoa huo zimebainisha kwamba umefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano kutoka 51 mwaka 2005 hadi vifo viwili 2019 katika kila vizazi hai elfu moja vinavyopatikana.
Mbali na kupata mafanikio makubwa katika kunusuru vifo vya akina mama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano, katika kipindi cha miaka 6 mkoa huo umefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka asilimia 14.8 hadi 11.6 jambo ambalo linamfanya Dr Ndugulile kushindwa kujizuia.
Aidha akiwa mkoani humo Dr Ndugulile ameambatana na mkuu wa mkoa huo Christopher Olesendeka kukagua ujenzi wa awamu ya pili wa majengo 12 ya hospitali ya rufaa wenye thamani ya bil 14.6 unaotekelezwa na kampuni ya MUST na kutoa agizo kwa mkandarasai kuongeza kasi ya ujenzi pamoja mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe kuongeza eneo la hospitali hiyo kwa kulipa fidia eneo linalotakiwa.
Baada ya agizo hilo ndipo mhandisi wa kampuni ya MUST inayotekeleza mradi huo Edson Rogasian anaitoa shaka serikali kwa kusema kwamba amejipanga vyema hivyo ana uhakika wa kumaliza kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa ili majengo hayo yaanze kunufaisha umma .
Naibu waziri wa afya maendeleo ya jamii ,jinsia wazee na watoto Dr Faustine Ndugulile yupo mkoani Njombe kwa ziara ya siku tatu ya kikazi.