Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku akiongea na Wanafunzi wa Sekondari na shule ya Msingi Mtinko iliyoko Wilaya Singida Jana Mkoani Singida.
Baadhi ya Walimu Shule ya Sekondari Mtinko iliyoko Wilaya Singida Jana Mkoani Singida wakifuatilia kampeini ya UKIMWI iliyotolewa Shuleni hapo jana na Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii.
***********************************
Na Mwandishi wetu SINGIDA
Viongozi wa Dini Mkoani Singida wameshitushwa na kiwango cha maambukizi ya UKIMWI hapa Nchini hasa kwa vijana na kuonya kuwa kama Taifa tusipokuwa makini na malezi kwa vijana Taifa litazidi kuangamia.
Viongozi hao wadini kwa nyakati Tofauti Mkoani Singida wamekili kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili kwa vijana unaosababishwa na uzembe wa malezi lakini pia wakitaja uwepo wa uwekezaji wa kumbi za starehe ambao haujasimamiwa kisheria kuwa unachangia maambukizi hayo.
Akiongea mapema leo ofisini kwake Kiongozi wa Kanisa Katoliki Mkoani Singida Askofu Edward Mapunda amesema watoto wa siku hizi hawana jipya la kujifunza kutoka kwa wazazi wao kutokana na wazazi hao kujikita zaidi katika kazi za kila siku na kushindwa kupata nafasi za kulea watoto lakini pia wazazi kushindwa kulinda ndoa zao na kuishi wakiwa wametengana.
Askofu Mapunda meongeza kuwa Kanisa linaamini mtu anaweza kuishi bila kufanya ngono kwakuwa ngono sio ugali, sio juisi, sio pilau wala sio tiba na hakuna aliyewai kufa kwa kukosa ngono na kuwataka watu kuwa na hofu ya Mungu ili waweze kuepukana na virusi vya ukimwi.
Aidha Askofu Mapunda alisema ni lazima kuwaeleza ukweli vijana kwamba wanaweza kuishi bila ngono kwa kuwa kwa Mungu hakuna msamaha kwani uwezi kumwambia Mungu kuwa umefanya ngono kwa kuwa haukuwa na sabuni akisisitiza kuwa ni bora ukaoga bila sabuni usipate ukimwi kuliko kupata ukimwi kwa kuoga na sabuni.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Watoto Kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maemdeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku akiongea na Vijana wa Shule ya Sekondari Kijota na Mtinko zilizoko Wilaya Singida alisema kuwa kila mwezi ukipita watu elfu sita wanapata maabukizi ya virusi vya UKIMWI nchini.
Aidha Bwana Kitiku aliongeza kuwa ni UKIMWI ni janga la Kitaifa kwani kila Siku ikipita watu 200 wanapata virusi vya ukimwi na kati ya watu hao maambukizi kwa vijana wa miaka 15-24 kwa siku ni 79 na kati ya hao 79 wasichana 63 hupata maabukizi mapya kwa Siku.
Naye Shekhe wa Mkoa wa Singida Shekhe Issa Simba akiongea ofisini kwake katika Manispaa ya Singida pia amesema kuwa kwa mujibu wa Kiongozi wa Dini hiyo Mtume Mohamed anasema kila ugonjwa una tiba yake lakini ugomjwa wa UKIMWI hauna tiba hivyo kuufananisha na adhabu na kuwataka watu kutubu na kumurudia Mungu.
Shekhe Issa Simba amewataka wazazi kumrudia Mungu na kulea watoto wao akionya kuwa tumeacha miiko ndio maana unakuta mtoto anakuwa wa mwisho kurudi usiku wakati wazazi wapo au mtoto namiliki simu kubwa kuliko mzazi lakini wazazi wanakaa kimya jambo ambalo linachangia upungufu wa maadili.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema kuwa Mkoa wa Singida ni lazima utokomeze maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kiwango cha asilimia sifuri akiwataka wadau wote mkoani kwake kuunganisha nguvu ili kutokomeza maradhi haya.
Aidha Dkt. Nchimbi alisikitishwa na ongezeko la maambukizi mkoani humo kwani takwimu zinaonesha kuwa maambukizi yameongezeka kwa kiwango cha asilimia 3.3 mpaka 3.6 jambo ambalo linakwamisha juhudi za Mkoa katika mapambano dhidi ya ukimwi.
Dkt. Nchimbi ameonya kuwa ni lazima kukomesha biashara ya ngono ulevi na makumbi ya starehe ambazo amezitaja kama visababishi vya maambukizi nakuwataka wamiliki wa vyombo hivyo kufikiria biashara nyingine vilevile akiwataka wafanya biashara ya ngono kuacha kabisa kwani hakuna mfanya biashara ya aina hiyo aliyewai kuacha urithi wa maana na wa kuigwa.
Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii iko Mkoani Singida kufanya kampeini kwa vijana kuhusu maambukizi ya ukimwi kampeini amabayo itaendelea kwa Mikoa ya Morogoro na Dodoma kama mikoa ya mfano na baadae Nchi Nzima kwa kushirikiana na TASAF, TACAIDS na kufadhiliwa na fedha ya Mfuko wa Dunia(Global Fund).