Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kati wa Shirika la Viwango Tanzania, Bi. Salome Emmanuel, akiwaonesha waandishi wa habari bidhaa zisizokidhi viwango na kuisha
muda wake wa matumizi wakati wa zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo lililofanyika leo Januari 16, 2020 katika dampo la Chidaya Jijini Dodoma.
Mtambo maalum unaotumika kuteketeza taka na bidhaa katika dampo la Chidaya Jijini Dodoma ukiendelea na kazi ya kuteketeza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi zilizokamatwa kwenye zoezi lililoendeshwa na Shirika la Viwango Tanzania kwenye mikoa ya Dodoma na Singida kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2019.
(Picha zote na MAELEZO)
******************************
Na Mwandishi wetu
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa kukosa kukidhi ubora.
Akizungumza wakati wa zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo zikiwemo vipodozi, vyakula na vinywaji, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kati ya Shirika hilo Bi. Salome Emmanuel amesema kuwa baadhi ya bidhaa zilizoteketezwa ni zile ambazo muda wake wa matumizi umekwisha na bado wafanyabiashara wasio waadilifu walikuwa
wakiendelea kuziuza.
“Ukaguzi tuliofanya kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2019 katika mikoa ya Dodoma na Singida umetuwezesha kubaini bidhaa hizi ambazo baadhi ya bidhaa zizisokidhi
viwango na nyingine muda wake wa matumizi umekwisha lakini bado wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiendelea kuziuza” alisisitiza Bi. Solome.
Akifafanua Bi. Solome amesema kuwa Shirika hilo litaendelea kufanya ukaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopo sokoni zinakidhi vigezo kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa wananchi wana jukumu la kushirikiana na shirika hilo katika kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wasio waadilifu hawafanikiwi kuuza bidhaa ambazo
muda wake umekwisha na ambazo hazikidhi vigezo.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara wote kuzingatia sheria na kanuni pale wanapotaka kuingiza bidhaa hapa nchini na hata wale wanaofanya uzalishaji hapa nchini.
Kwa upande wake mkaguzi wa Chakula wa Shirika hilo Bw. Abel Deule amesema kuwa Shirika hilo linaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wanalindwa dhidi ya bidhaa zisizo na ubora na zile ambazo muda wake wa matumizi.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa likifanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingia nchini zinakidhi vigezo.