Mkurugenzi Mtendaji wa tiba wa hospitali ya rufaa ya Haydom Mkoani Manyara, Dkt Emmanuel Nuwass akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 64 ya hospitali hiyo ambapo vifaa tiba vya shilingi bilioni 1.6 vilizinduliwa.
*******************************
HOSPITALI ya rufaa ya Haydom Mkoani Manyara, imesherehekea maadhimisho ya miaka 64 tangu ianzishwe kwa kuzindua vifaa tiba vya thamani ya shilingi bilioni 1.6 vya hospitali hiyo.
Hospitali ya rufaa ya Haydom ya Kilutheri inayomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Mbulu ilianzishwa mwaka 1955 na wamisionari wa Norway ina vitanda 420 baada ya kupandishwa hadhi mwaka 2010.
Hospitali hiyo inashirikiana na serikali ya Tanzania kupitia halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Maadhimisho hayo yalitarajiwa kuwa na mgeni rasmi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu lakini akawakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Simbalimile Mofuga.
Mofuga alisema mzigo mzito huwa anapewa mnyamwezi hivyo yeye amekasimiwa madaraka na Waziri Wa Afya ili amwakilishe kwenye tukio hilo kubwa la kihistoria.
Alisema kila wakati anaimwagia sifa hospitali hiyo kwani inabeba taswira nzuri ya wilaya kutokana na huduma bora na nidhamu iliyopo.
“Hivi sasa mnazidi kupiga hatua mnapaswa kuandika barua upya ili hospitali ipandishwe hadhi kuwa ya kanda kwani inatoa huduma kwa watu wengi na walio na hali duni,” alisema Mofuga.
Alisema uongozi wa hospitali hiyo ni wabunifu kwani wamefanikisha ununuzi wa vifaa hivyo kwa kuendesha harambee na kuchangiwa na wadau wa maendeleo.
Mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya rufaa ya Haydom, Dk Emmanuel Nuwass alisema vifaa tiba hivyo vinne vipya vilivyozinduliwa vimegharimu shilingi bilioni 1.6.
Dk Nuwass alisema vifaa hivyo ni CT scan, digital X-ray, mtambo wa kuzalisha hewa ya oxsijeni kwa ajili ya wagonjwa na mashine ya kisasa ya kuteketeza taka hatarishi.
Alisema mashine ya CT Scan ya kampuni ya Siemens yenye thamani ya shilingi milioni 654.2 ikiwa imeshawahudumia zaidi ya wagonjwa 250, mashine ya pili ni Digital X-ray ya kampuni ya GE Health care ya thamani ya shilingi milioni 320.2 mashine ya kuzalisha hewa ya oxsijeni ya kampuni ya Ozcan Kardelser ya thamani ya shilingi milioni 372.9 imezalisha mitungi 1,665 imeokoa shilingi milioni 72 zilizokuwa zimetumika na mashine ya kuteketeza taka hatarishi (Incinerator) yenye uwezo wa kuchoma kilogramu 100 ya taka kwa saa yenye thamani ya shilingi milioni 203.
Alisema hospitali ya rufaa ya Haydom inahudumia wagonjwa 105,296 wa nje na 14,020 wa ndani kwa mwaka kwenye mikoa ya Manyara, wilaya ya Karatu mkoani Arusha, wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wilaya za Mkalama na Iramba Mkoani Singida na wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Mwakilishi wa Balozi wa Norway nchini, Britt Hilde Kjolas alisema kwa zaidi ya miaka 60 kabla ya uhuru nchi yake ilikuwa na ushirikiano mkubwa na Tanzania hadi sasa.
Mkurugenzi mkazi wa Norwegian Church Aid (NCA) Gwen Bwerge aisema Serikali izidi kuweka mkono wake kwa kuongeza watumishi kwani hivi sasa vifaa vipo.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mbulu, Nicolaus Nsangazelu alisema kuna baadhi ya wagonjwa kutoka wilayani Meatu mkoani Simiyu ambao aliwauliza mbona wamekuja kutibiwa mbali wakadai wamefuata huduma bora.
Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Maasay alisema aliwahi kuwakutanisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na uongozi wa hospitali hiyo ili kuzungumzia changamoto zilizopo hospitalini hapo.