Umoja na mshikamano uliopo baina ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, vimetajwa kuwa ndio chanzo cha mafanikio waliyo yapata katika kusimamia suala la afya ikiwepo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo hadi sasa wamefikia asilimia 90 ya ujenzi baada yakupokea shilingi bilioni 1.5 kutoka Serikali kuu kwaajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Said Mtanda, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Namigogo pamoja na Mkurugenzi wa Halamashauri hiyo Misana Kwangula, wameeleza kwamba, muda mwingi wamekuwa wakiutumia kukutana eneo la kazi na imekuwa kama desturi kwenda eneo la kazi mara tatu kwa siku. Mkuu wa Wilaya hiyo amesema asipokuwepo yeye basi atakuwepo Mganga Mkuu au Mkurugenzi hivyo wakafanikiwa kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliowekwa na Serikali.
Akizungumza akiwa katika eneo inapojengwa Hospitali hiyo, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kutokana na kufanya vizuri kama zilivyo Hospitali za Wilaya za Ilemela ya Mwanza na Bahi mkoani Dodoma ambao kwa asilimia kubwa wamefikia asilimia 90 Halmashauri hiyo, itapatiwa fedha zakukamilisha ili waanze kutoka huduma kwa wananchi.
Aidha Dkt. Gwajima, ametumia fursa hiyo kuzionya Halmashauri ambazo zimeshindwa kufikia asilimia 90 huku zikiomba kuongezewa fedha amesema, itabidi zitoe maelezo ya kina juu yakile walicho kitekeleza hadi sasa kabla yakufikiriwa katika mgao mpya.
“Hapa lazima tuelewane, wale ambao wameshindwa kufikia asilimia 90 lazima watoe uafafanuzi, iweje Nkasi waweze, Ilemela waweze, halafu huko kwingine ishindikane? Alihoji Dkt. Gwajima na kusema kwamba wao hawata watesa wananchi, bali watapeleka huduma lakini wahusika lazima wawajibike kila mmoja kwa eneo lake. Alihitimisha Naibu Katibu Mkuu huyo anayeshughulikia Afya kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI. (Imeandaliwa na Atley Kuni- Afisa habari Ofisi ya Rais TAMISEMI)