Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage (kulia) akimkabidhi zawadi ya saa yenye nembo ya NEC, kiongozi wa Ujumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo, JajiDkt. Jane Ansah.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) JajiRufaa (Mst) Semistocles Kaijage (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) Jaji Dkt. Jane Ansah ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage akifungua kikao baina ya Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) na NEC Jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk na kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) Jaji Dkt. Jane Ansah.
Viongozi wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Malawi (MEC) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Tume hizo na maafisa waandamizi leo Jijini Dar es salaam mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina ya MEC na NEC.
Picha na Idaraya Habari na Elimu ya Mpiga Kura-NEC
*********************************
Dar es salaam, 13 Januari, 2020
Ujumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) leo (Jumatatu) umefanya ziara ya
kikazi kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa lengo la kubadilishana uzoefu
juu ya mambo mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa chaguzi.
Ujumbe huo wa watu 11 ambao umeongozwa na Mwenyekiti wa MEC Jaji Dkt. Jane Ansah
umekutana na kufanya mazungumzo na Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu
masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa uchaguzi katika nchi hizi mbili.
Akizungumza katika kikao cha pamoja baina ya Tume hizo mbili, Mwenyekiti wa NEC Jaji Rufaa (Mst.) Semistocles Kaijage ameonyesha kufurahishwa kwake kwa Tume ya Uchaguzi ya Malawi kuitembelea NEC ili kubadilishana uzoefu.
Amesema.“Tanzania na Malawi ni wanachama wa umoja wa Tume za Uchaguzi wa nchi za SADC ambao mojawapo ya malengo yake ni kujengeana uwezo katika kusimamia chaguzi. Nafurahi kuona mmechagua kuja Tanzania ili kujifunza na kubadilishana uzoefu”
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi Jaji Dkt. Jane Ansah ameishukuru NEC kwa kufanikisha kikao hicho cha pamoja kwani masuala mengi ya msingi yameweza
kujadiliwa.
Amesema “mazungumzo haya yameibua masuala mengi ya msingi kwa pande zote mbili. Sisi tunaondoka hapa tukiwa na uelewa mpana zaidi wa masuala haya yahusuyo
usimamizi wa chaguzi hasa taratibu za ugawaji wa majimbo ya uchaguzi”.
Ujumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi unajumuisha Mwenyekiti wa Tume, Makamishna 5, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Maofisa wengine 4.