***************************
Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana Jumatatu tarehe 13 hadi 24 Januari, 2020 Jijini Dodoma kutekeleza majukumu ya kibunge kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 28 Januari, 2020.
Kwa mujibu wa Ratiba ya Shughuli za Kamati, Waheshimiwa Wabunge wanapaswa kuwasili Jijini Dodoma Jumapili tarehe 12 Januari, 2020 tayari kwa ajili ya kuanza kwa vikao vya Kamati. Aidha, Shughuli zote za Kamati zimepangwa kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.
Shughuli zitakazotekelezwa na Kamati hizo ni pamoja na:-
a) Kupokea na Kujadili Taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Majukumu na Bajeti ya Serikali kupitia Wizara na Taasisi zake. Shughuli hii itatekelezwa na Kamati za Kisekta na Bajeti.
b) Kushughulikia hoja mbalimbali za Ukaguzi kama zilivyoripotiwa katika Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha unaoishia Juni, 2018. Jukumu hili litatekelezwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
c) Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) itafanya ziara za ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika baadhi ya miradi ya maendeleo.
d) Kupokea taarifa kuhusu namna hisa za Serikali zinavyosimamiwa katika mashirika na Taasisi mbalimbali ambazo Serikali ina hisa pungufu ya asilimia hamsini. Shughuli hii itatekelezwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
e) Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Mezani wakati wa Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge. Shughuli hii itatekelezwa na Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo.
f) Kuandaa taarifa ya Kamati kuhusu shughuli zilizotekeleza katika kipindi cha kuanzia Januari, 2019 hadi Januari, 2020. Shughuli hii itatekelezwa na Kamati zote.
Ratiba za Shughuli za Kamati za Bunge pamoja na maeneo ambayo Kamati hizo zitafanya ziara zinapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz.