Na Said Said Nguya
Desemba 23 mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.
Bashiru Ali alianza likizo ya mwaka kwa siku Kumi, ambapo mpaka
Januari 03 mwaka huu alikuwa nyumbani kwao Bukoba vijijini, mkoani
Kagera.
Ameshuhudiwa akitumia muda mwingi wa mapumziko yake, katika shughuli
mbalimbali za kijamii na kisiasa, akitoa ufafanuzi na maelekezo
mbalimbali kwa lengo la kuimarisha zaidi Chama hicho.
Kupitia mkutano wa ndani wa wenyeviti wa mitaa na vijiji wilayani
Bukoba, Dkt. Bashiru alitoa msimamo wa chama katika kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi mkuu, mwishoni mwa mwaka huu, kwamba CCM kitafanya
siasa safi, kikiheshimu maamuzi ya Umma kama ambavyo kimekuwa
kikifanya kwenye chaguzi nyingine.
Dkt. Bashiru pia alitumia mkutano huo kutoa ufafanuzi kuhusu hoja
mbalimbali za vyama vya upinzani, ikiwamo ile ya madai ya tume huru ya
uchaguzi.
Alielezea hoja hiyo kuwa haina mashiko kwani jukumu kuu la tume ya
uchaguzi, ni kusimamia uchaguzi si vinginevyo kwahiyo, chama
kisipokuwa na wapiga kura, tume ya uchaguzi haiwezi kukisaidia kupata
ushindi.
“CCM kinaendelea kutafuta wapiga kura kwa kusomesha wanafunzi bure,
kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuboresha na kuimarisha
huduma za kijamii ikiwamo kujenga vituo vya afya, barabara sasa,
huduma za maji na umeme…, sasa wao waseme wanatumia njia gani kupata
wapiga kura na wanawafanyia nini wapigakura wao?,” alisema Dkt.
Bashiru.
Alitamba kuwa mpaka sasa CCM ndicho pekee kilichoweka wazi msimamo
wake wa kupinga udharirishwaji na ubaguzi wa wanawake, katika ngazi
tofauti za uongozi.
“Mara nyingi imeshuhudiwa wanawake kabla ya kugombea wakiitwa majembe,
kwenye vyama Fulani vya siasa lakini wakichukua fomu kwa ajili ya
kugombea nafasi za uongozi, wanachimbwa na kuwekewa kashfa nyingi,
wanatishwa na hata kufanyiwa mambo ya hovyo, awamu hii CCM
hakitakubali wamawake wadharirishwe,” alisema.
Akizungumzia mchakato wa kupata wagombea ndani ya chama hicho, Dkt.
Bashiru, alikemea tabia ya baadhi ya wanaCCM kuabudu majina ya watu,
kwa imani kuwa majina ya watu hao yasipopitishwa kugombea chama
haiwezi kushinda.
Hatua hiyo imeibua ari mpya miongoni mwa wanaCCM wa maeneo mbalimbali
nchini, ikiwemo Jimbo la Bukoba mjini, ambalo ni sawa na Jimbo lisilo
na mwakilishi kufuatia Mbunge wake, Alfred Lwakatare kutokuwa karibu
na wananchi kwa muda mrefu, huku chama chake cha Chadema kikikosa
mvuto kisiasa jimboni huo.
Alipotembelea na kukagua ujenzi wa ofisi ya chama hiko kwenye Kata ya
Bwanjai, wilayani Misenyi Dkt. Bashiru alitaka wananchi kupuuza baadhi
ya sera na kauli za viongozi wa vyama vya siasa, zinazolenga kurejesha
nyuma maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Viongozi tunaongoza mapambano ya kujikomboa kiuchumi, kila mtu
anahitajika kuhimiza kufanya kazi kwa bidii, kwamfano CCM tuna kauli
mbalimbali za kuhimiza hilo ikiwamo, Hapa Kazi tu, Kazi na Maendeleo,
Uhuru na Kazi pamoja na ile ya Kazi ni Utu, ajabu ni kwamba kuna vyama
vinahubiri kazi na starehe…, hapa ndipo mnapoweza kuona tofauti kati
ya chama kiongozi na vyama vya uchaguzi,” alisema Dkt. Bashiru.
Kauli za aina hiyo alizitafsiri kuwa kauli za kipumbavu, akaomba
watanzania kuzidharau kwasababu zinatolewa na viongozi wasiokuwa na ni
njema na taifa, wenye hulka ya kulaghai umma kwa kutumia siasa
nyepesi.
Nao viongozi wa chama na serikali, walipewa maagizo anuai ikiwamo
agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya, kuhakikisha wafanyakazi, wahudumu
na mafundi kwenye miradi yote inayotekelezwa na serikali, ambayo
imeishapelekewa fedha na serikali kuu wanalipwe haki zao kwa wakati.
Agizo hilo lilifuatia hatua yake ya kukagua mradi wa ujenzi hospitali
ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, ambao pamoja na kuwa katika hatua
za mwisho, alipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa mradi huo
kwamba hawakuwa wamelipwa fedha zao.
Dkt. Bashiru pia alihimiza utekelezwaji wa azimio la Halmashauri Kuu
ya Taifa, linalotaka kamati za siasa za mikoa na wilaya, kuwasilisha
maoni yao kabla ya Januari15 mwaka huu, kwa ajili ya kukamilisha
Ilani ya uchaguzi na mwelekeo wa Sera za CCM 2020-2030.
Alivitaka na vyama vya upinzani pamoja na makundi mengine ya kijamii,
kutoa maoni yao ili yaingizwe kwenye ilani ya CCM kwasababu kutokana
na kasi ya uongozi na ubora wa huduma zinazotolewa na serikali
inayoongozwa na chama hicho, hakuna ubishi kwamba kitashinda katika
uchaguzi mkuu ujao, baadaye mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa, katika Kikao cha Halmashauri kuu ya Taifa iliyofanyika Desemba, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, alitoa hotuba ya ufunguzi wa semina ya Wajumbe hao iliyoonekana kusisimua wajumbe kwa kugusa maeneo yote muhimu ya maendeleo, na Makaku mwenyekiti wa CCM Zanzibara na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein alitoa hotuba ya kufunga, ambazo hotuba zote mbili ziliamuliwa ziwe ndio miongozo katika uandishi wa Ilani na Mwelekeo wa sera wa Chama hiko kongwe barani Afrika
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kuzindua makazi ya Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amoni Mpanju, kwenye Kijiji cha
Nyakibimbili, aliasa jamii kusaidia watu wenye ulemavu ili waweze
kung’amua fursa, kupitia vipawa vyao kama ilivyofavyika kwa Mpanju.
“Inatakiwa tuwapende zaidi watu ambao kwa maumbile yao hawawezi
kutenda baadhi ya mambo bila msaada, lakini wanavipawa vya kusaidia
jamii yao na nchi kwa ujumla, Amoni ni miongoni mwa watu wanaotusikia
lakini hawatuoni…, namfahamu vizuri, ni miongoni mwa vijana wachapa
kazi zaidi hata ya wanaoona, majukumu aliyonayo hajapewa kwa upendeleo
bali anayamudu sawasawa,” alisema Dkt. Bashiru.
Pia alihimiza zaidi upendo kwa watoto, akisema CCM kimeonesha njia kwa
kuweka utaratibu wa elimu bila malipo, kwamba watoto wengi wamepata
fursa ya kupata elimu tofauti na awali.
Naye Mpanju, akizungumza wakati akimkaribisha Dkt. Bashiru alielezea
ugumu aliyokabiliana nao katika maidha yake, ikiwamo kufiwa na wazazi
wake wote wawili akiwa katika umri mdogo, hali iliyosababisha
asomeshwe na watu ambao baadhi hakuwa akiwafahamu.
Pamoja na watu hao, alishukuru itikadi ya Ujamaa akisema bila itikadi
hiyo iliyojenga na kueneza udugu na ujamaa miongoni mwa watanzania,
ana uhakika asingesoma.
Mwandishi ni Mchambuzi wa siasa na maendeleo nchini.