Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akimsalimia mzee ambaye hajiwezi katika Makao ya Wazee Magugu Mkoani Manyara mara baada ya kutembelea Makao hayo jana kwa lengo la kuongea na wazee waishio katika Makao hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akimsalimia na baadhi ya wazee wanaotunzwa na kuishi katika Makao ya Wazee Magugu Mkoani Manyara mara baada ya kutembelea Makao hayo jana kwa lengo la kuongea na wazee waishio katika Makao hayo.
Baadhi ya Wazee wanaoishi katika Makao ya Wazee Magugu wakiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. jana alipotembelea Makao hayo jana kwa lengo la kuongea na wazee waishio katika Makao hayo.
………………
Na Anthony Ishengoma
Serikali itaendelea kuboresha na kukarabati miundombinu ya Makao yote ya Wazee wasiojiweza hapa Nchini kwa lengo la kuhakikisha wazee wote ambao wamekosa huduma katika familia na jamii wanaendelea kuishi katika mazingira bora na salama katika Makao yote yanayomilikiwa na Serikali.
Akiongea na Wazee wanaoishi katika Makao ya Wazee ya Magugu Mkoani Manyara jana Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu aliwaambia wazee hao kuwa Serikali inafanya ukarabati na kujenga majengo kwa lengo la kuhakikisha wazee hao wanaishi katika makao yenye staha.
Akiongea na Wazee Dkt. Jingu aliongeza kuwa pamoja na misaada kutoka kwa wasamalia wema Serikali inagharimia chakula cha wazee pamoja na kuwapatia huduma za afya ili kulinda na kuboresha afya zao kwa muda wote wawapo katika makao hayo yanayomilikiwa na Serikali.
Aidha Dkt. Jingu aliwataka wazee hao pamoja na wafanyakazi wanaohudumia wazee hao kuhakikisha wanatunza nyumba za makao ya wazee hao ili nazo ziweze kuwatunza akiwasisitiza kuahakikisha wanalinda miundombinu yote ya makao ya wazee.
Dkt. Jingu pia ameitaka Jamii ya Watanzania kutambua kuwa jukumu la kutunza Wazee sio la Serikali bali ni jukumu la watoto, na familia ya mzee husika na kuitaka jamii kuhakikisha inalinda na kuwatunza wazee kwani jukumu la msingi kwa familia kutunza wazee.
‘’Tunapata maombi ya kuwatunza wazee kutoka kwa watu ambao kimsingi wana wajibu wa kuwatunza wazee na kuwambia hapana jukumu la msingi la kutunza wazee ni la familia’’. Alisisitiza Dkt. Jingu’’.
Dkt. Jingu alizitaza sifa za mzee anayepaswa kutunzwa katika Makao ya Taifa ya Wazee kuwa ni yule mzee ambaye kwa namna yoyote ile amekosa ndugu wa kumtunza na kumlea na hana makazi maalum ya kuishi lakini pia akiwataka wazee wote wanaoishi katika makao kufuata taratibu za Serikali zilizowekwa ili kuendelea kuishi katika makao hayo.
Katibu Mkuu Jingu tayari ametembelea Makao ya Wazee Njilo Mkoani Kilimanjaro na kuzungumza na wazee wanaoishi katika Makao hayo lakini pia kuangalia ukarabati wa makao hayo unaoendelea katika Makao hayo yaliyoko katika Manispaa ya Moshi.