Na Emmanuel J. Shilatu
Heri ya Mwaka mpya 2020 Ndugu yangu Mtanzania. 2020 ni Mwaka mwingine wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anaendelea kuongoza. Naam! Watanzania tumemchagua Rais Magufuli aendelee kuongoza 2020 ili tuone kazi aliyoianza inakamilika ipasavyo na Watanzania wananufaika na matunda ya kazi hiyo.
(i) Kuhamia Dodoma
Wazo la Serikali kuhamia kwenye makao makuu ya nchi mkoani Dodoma liliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwaka 1973 lakini lilishindwa kutekelezwa katika awamu zote. Si awamu ya kwanza, wala ya pili, ama ya Tatu au ya nne bali limeweza kufanikiwa kwenye utawala wa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli. Leo hii karibia Serikali yote imehamia Dodoma. Wizara, taasisi na idara za Serikali, Waziri Mkuu wameshahamia Dodoma mpaka Rais Magufuli naye amehamia Dodoma. Iliasisiwa na Mwalimu Nyerere, ikahaidiwa kwenye ilani ya uchaguzi, imekuja kutekelezwa vyema na Rais Magufuli lakini uhamiaji huu ni kwa awamu awamu. 2020 Watanzania tumemchagua Rais Magufuli akaimalizie hii kazi iliyokwama hapo awali bali yeye ameiweza kwa kuhakikisha Serikali kamili pamoja na idara zake zinahamia Dodoma.
(ii) Ujenzi wa Stiegler’s Gorge ama Mto Rufiji
Utawala wa awamu ya kwanza uliokuwa ukiongozwa na Mwalimu Nyerere ulikuja na wazo la kujenga Stiegler’s Gorge mnamo mwaka 1981 lakini umeshindwa kufanyika mpaka awamu hii ya 5 inayoongozwa na Rais Magufuli umeamua kufufua na kuliendeleza wazo hili ambalo pasipo ushujaa na ujemedari wa Rais Magufuli basi usingefanyika. Mradi wa Stiegler’s Gorge kupitia Mto Rufiji utafanikiwa kuzalisha Megawattz 2115 hadi utakapo kamilika ambapo utakuwa umeme mkubwa kuzidi huu unaotumika sasa. 2020 Watanzania tumemchagua Rais Magufuli ahakikishe ukamilifu wa mradi huu ambao utajenga uhakika wa umeme nchini, utashusha bei ya umeme nchini na pia utasaidia kuimarisha sekta ya viwanda nchini. Ni kwa uwepo wa uongozi imara wa Rais Magufuli pekee atasimamia vyema ukamilifu wa mradi huu ambao ni mkombozi wa umeme mjini hadi vijijini.
Pamoja na changamoto zote Dkt Kalemani: Hadi kufikia leo vijiji 8,818 kati ya vijijini 12,000 nchini vimepata umeme kutoka vijiji takribani 2,000 ushee tu vilivyokuwa na umeme 2015. Mwaka 2020 tumemchagua Rais Magufuli akamilishe kazi ya kusambaza umeme vijiji vyote nchini vilivyosalia.
(iii) Ujenzi wa reli ya kisasa (SGR)
Ni takribani miaka 120 ambapo historia iliandikwa mwaka 1912 kwa Serikali ya kikoloni kujenga Reli inayotumia dizeli. Leo hii kwenye sekta ya reli Rais Magufuli amefanya makubwa. Kwanza amefufua usafiri wa Dar – Moshi uliokuwa umekufa kwa zaidi ya miaka 25; Ameimarisha usafiri wa reli wa Dar – Dodoma – Kigoma ambapo sasa ni wa uhakika zaidi.
Tuachane na hayo, kuna hili la ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha Standard gauge (SGR) ambapo awamu ya kwanza imeanzia Dar – Morogoro na baadae Morogoro – Dodoma na kumalizia Dodoma – Mwanza kukamilisha umbali wa Kilomita 1219.
2020 Watanzania tumemchagua Rais Magufuli ahakikishe ukamilifu Reli hiyo ulete tija kwenye usafirishaji, Kilimo, utalii, uzalishaji na kibiashara. SGR itakuwa na uwezo wa kubeba tani milioni, 10,000, kwa mkupuo sawa na malori 500 yenye tani 20, Treni tano zenye tani 10,000 na kuwa na kasi kubwa ya 160km/saa, tofauti na ya sasa ambayo inakasi ya 30km/saa, kwa Afrika itakuwa ni Reli pekee yenye uwezo mkubwa kama huo, tani Miliomi 10-17 zitasafirishwa kwa mwaka, kwa hiyo SGR ni mwamba sekta ya usafirishaji nchini.