Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. Aidha katika kipindi cha sikukuu ya mwaka mpya hali ya usalama ilikuwa shwari, ulinzi uliimarishwa katika maeneo yote na wakazi wa Mkoa huu na wageni walisherehekea kwa amani na utulivu.
TAARIFA YA KUKUTWA JENEZA SOKONI SOWETO.
Ni kwamba mnamo tarehe 21/12/2019 mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MASUOD MUSA MOHAMED [47] mfanyabiashara na mkazi wa makambako mkoani Njombe aliletwa kwa gari ya wagonjwa [Ambulance] katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na mnamo tarehe 23/12/2019 majira ya 05: 00 alfajiri mtu huyo alifariki dunia na ndipo mmoja wa ndugu yake aitwaye HAMIS MUSSA HAMAD [61] mkazi wa Pambogo Iyela Jijini Mbeya aliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika msikiti wa MASJID TAUFIQ uliopo Block Q Soweto kwa ajili ya kuoshwa na kuswaliwa ambapo baada ya shughuli hizo kukamilika mwili wa marehemu ulihifadhiwa kwenye jeneza lililokuwa msikitini hapo na kisha kusafirishwa kuelekea Makambako kwa mazishi ambapo siku hiyo hiyo majira ya saa 18:00 jioni ulizikwa.
Baada ya kumaliza mazishi jeneza hilo lilibaki kwenye msikiti wa Makambako baada ya kukosa usafiri wa kulirudisha Mbeya kwa siku hiyo. Mnamo tarehe 31/12/2019 ALLY MOHAMED Mkazi wa Makambako alimkabidhi jeneza dereva wa lori ili aweze kulileta hapa Mbeya na kumpatia namba ya simu ya HAMIS MUSSA HAMAD ili alipokee jeneza hilo. Aidha lori hilo lilikuwa limebeba mzigo wa nyanya ambapo baadhi zilikuwa zinashushwa soko la Soweto na zingine zinapelekwa Songwe, hivyo majira ya saa 01:00 usiku wa kuamkia tarehe 01.01.2020 dereva huyo alifika Soweto na kushusha nyanya pamoja na jeneza lakini alipompigia HAMIS MUSA HAMAD mtu ambaye aliyeambiwa kuwa atalipokea jeneza hilo hakuweza kupatikana hewani hivyo ilimlazimu dereva huyo kukaa mpaka saa 04:00 usiku wa tarehe 01.01.2020 bila mafanikio na ndipo aliamua kumuachia mmoja wapo wa walinzi wa sokoni hapa ili ikifika saa 05:00 alfajiri kipindi cha swala aweze kuwakabidhi jeneza msikitini hapo.
Sambamba na hilo alimuachia namba ya simu ya mpokeaji kwa ajili ya mawasiliano na kisha dereva aliondoka kwenda Songwe lakini mlinzi huyo alilitelekeza jeneza hilo pale liliposhushwa na kuondoka zake hali iliyosababisha taharuki kwa wafanyabiashara wa soko hilo pamoja na wakazi wa eneo hilo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, limefuatilia kwa karibu suala hili na nitumie nafasi hii kukanusha habari zilizokuwa zimeenea kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitando ya kijamii kwani uhalisia wa suala hilo ni huu, hivyo niwatake wafanyabiashara na wananchi wa mkoa wa Mbeya kuendelea na kazi/biashara zao kama kawaida.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUGHUSHI NYARAKA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia ABRAHAM OBEDI [55] wakala wa bima ya GTM na Mkazi wa Isanga Jijini Mbeya akiwa na mihuli hamsini na sita [56] ya idara mbalimbali za serikali na ofisi binafsi ambayo imeghushiwa na kuhifadhiwa katika ofisi yake ya Stationaries.
Mtuhumiwa alikamatwa Disemba 31, 2019 majira ya saa 17:00 jioni huko maeneo ya Mtaa wa Sokoine uliopo Kata na Tarafa ya Sisimba Jijini Mbeya baada ya Jeshi la Polisi Mkoani hapa kupata taarifa na kisha kufanya msako mkali na kufanikiwa kumtia nguvuni mtuhumiwa pamoja na vielelezo.
Baadhi ya mihuli na nyaraka alizokutwa nazo mtuhumiwa ni kama ifuatavyo:-
- Mhuli wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Soko Kata ya Ruanda,
- Mhuli wa Afisa biashara wa Halmashauri ya Mbeya,
- Access Bank Tawi la Mbeya,
- Mamlaka ya Mapato Mbeya [TRA]
- Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini,
Aidha mtuhumiwa alikutwa pia na Kompyuta moja aina ya Accer, Stika za bima, Poss Machine na nyaraka mbalimbali vikiwemo vyeti vya wanafunzi ambao vimeghushiwa. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
KUPATIKANA NA BHANGI.
Jeshi la Polisi Mkoani hapa linamshikilia AGREY MASHAKA @ MBOTO [25] Mkazi wa Kilambo Wilayani Kyela akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kavu kilogramu thelathini [30].
Mtuhumiwa alikamatwa Disemba 31, 2019 majira ya saa 14:45 mchana baada ya Jeshi la Polisi Mkoani hapa kufanya msako mkali huko Kitongoji cha Kilambo, Kata ya Njisi, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela na Mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa bangi hiyo.
Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.