******************************
Mnamo tarehe 28.12.2019 majira ya saa 21:00 usiku Huko maeneo ya Mtaa wa Shewa, Kata ya Mwakibete, Tarafa ya Iyunga, Jijini mbeya. MASHAKA JUMA aligundua kupotelewa na watoto wake wawili ambao ni FAISAL MASHAKA, miaka mitano , mwanafunzi wa Shule ya Juhudi Day Care Centre na FARHANA JUMA, mwaka mmoja na miezi mitano wote wakazi wa Shewa.
Ni kwamba siku ya tarehe 28.12.2019 majira ya jioni watoto hao walikuwa wanacheza jirani na nyumbani kwao na ndipo walipotea. Juhudi za kuwatafuta zinaendelea.
KUELEKEA SIKUKUU YA MWAKA MPYA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuelekea sikukuu ya mwaka mpya 2020 kwa kufanya doria na misako ya uhalifu pamoja na ile ya usalama barabarani hasa katika maeneo tete kama vile ya mlima Iwambi, mlima nyoka, mlima mwansekwa na mlima igawilo.
Jeshi la Polisi pia limepiga marufuku upigaji wa fataki kipindi hiki cha sikukuu [sherehe] ya mwaka mpya hasa katika mkesha na linawataka wananchi wote kusherehekea sikukuu hii kwa amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo vya uchomaji moto matairi ya magari barabarani kwani husababisha
uharibifu mkubwa wa barabara na kulisababishia taifa hasara kubwa, hivyo limejipanga vizuri kuhakikisha hakuna vitendo kama hivyo.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi linawataka watumiaji wote wa vyombo vya moto kujiepusha na matumizi ya vilevi kama vile pombe na matumizi ya dawa za
kulevya kwani kutakuwa na askari wakutosha katika maeneo yote kuhakikisha madereva wanapimwa kilevi na endapo watabainika kutumia kilevi
watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani.
Aidha katika kipindi hiki cha sikukuu, ni wito wa Jeshi la Polisi kwa wazazi na walezi kuwa makini zaidi ya kawaida kwa watoto wao, kuweka uangalizi wakutosha katika maeneo tofauti tofauti kama vile nyumbani, makanisani,
misikitini na sehemu za michezo ya watoto ili kuepuka matukio ya kupotea kwa watoto pamoja na madhara yanayoweza kuwapata watoto pindi wanapokosa
uangalizi wa karibu toka kwa mzazi au mlezi.
Mwisho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya kwa niaba ya Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi, anawatakia wananchi wote wa mkoa wa Mbeya na Watanzania kwa ujumla Kheri ya Mwaka Mpya 2020 huku akiwataka kukumbuka kufanya vitu kwa kiasi, bila kuvuka viwango/mipaka.