Home Mchanganyiko LORI NA BASI YAGONGANA WATU 6 WAFARIKI DUNIA JIJINI DODOMA

LORI NA BASI YAGONGANA WATU 6 WAFARIKI DUNIA JIJINI DODOMA

0

WATU sita wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa baada ya lori na basi dogo la abiria kugongana jana Jumapili, majira ya saa nne usiku jijini Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kwamba chanzo chake ni dereva wa lori kukwepa korongo katikati ya barabara.

“Lakini wakati anahama kukwepa korongo hilo, tayari lile basi dogo la abiria lilikuwa limeshafika karibu, na bodi la lori likaliangukia basi hilo la abiria na kusababisha vifo na majeruhi. Tunaendelea kumsaka dereva wa lori kwani alikimbia usiku ule baada ya tukio hilo,” amesema Muroto.

Mganga Mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma, Dr. Elinesti Ibenzi, amethibisha kupokea miili sita ya marehemu wa ajali hiyo na majeruhi 12 ambao wamelazwa na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.