Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally, amewaomba wananchi kupuuza sera na kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini zikitaka wananchi wale bata (wafanye starehe) badala ya kufanya kazi jambo ambalo likiachwa bila kukemewa litafanya kuwa na taifa legelege la kupenda starehe badala ya kazi.
Dkt. Bashiru amesema kuwa, katika nchi ambayo wananchi wanapambana kujikomboa kiuchumi, hasa katika nchi zetu za Afrika ambazo bado tupo nyuma kimaendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, kutokea kiongozi mmoja kuwaambia watu wafanye kazi kwa starehe ni usaliti mkubwa wa mapambano ya kiuchumi ambayo kama taifa tunayahimiza.
Katibu Mkuu ameyasema hayo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Bwanjai wilayani Misenyi tarehe 28 Desemba, 2019 na kuzungumza na wanachama na wananchi waliojitokeza katika ukaguzi huo.
“Nchi hii ambayo tunaongoza mapambano ya kujikomboa kiuchumi, inamuhitaji kila mtu kwa nafasi yake kuhimiza kufanya kazi kwa bidii, na huku CCM kuna kauli mbalimbali za kuhimiza kazi zikiwemo, Hapa Kazi tu, Kazi na Maendeleo, Uhuru na Kazi na Kazi ni Utu, ila kuna baadhi ya Vyama wao wanahubiri kazi na starehe, na huo ndio utofauti wa Chama kiongozi na Vyama vya uchaguzi.’’ Dkt. Bashiru ameeleza
Ameongeza kwa kusisitiza kuwa, “Unaposema kazi na bata, maana yake ni kudharirisha wanawake na mama zetu ambao wakati wote wamekuwa wakifanya kazi kusomesha watoto wao, wakifanya kazi kulisha familia zao, na sote hapa ni matokeo ya juhudi kubwa za mama zetu, ambao kuwambia wale bata, ni sawa na kuwataka washinde kwenye starehe huku watoto wakidharirika kwa kutokwenda shule, hizi ni kauli za kipumbavu za Vyama vya uchaguzi, ambazo hatuna budi kuzidharau na kuzipuuza.”
Aidha ameongeza kuwa, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwa chama cha kutetea haki za wanyonge na kitaendelea kusisitiza sekta zote za serikali zikiwemo afya, elimu, miundombimu na maji kutoa huduma kwa wananchi bila usumbufu wala ubaguzi na kuthamini utu wa watu wote.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera mama Costancia Buhiye na Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanal Mstaafu Denis Mwila
Ikumbukwe kuwa, Dkt. Bashiru yupo nyumbani kwake Bukoba mkoani Kagera kwa mapumnziko ya siku kumi, na anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mapema mwezi Januari, 2020.