Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira Mhe. George Simbachawene amekemea watu wanaojihusisha na vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umma na ya watu binafsi ili kwenda kuuza kama chuma chakavu kuacha mara moja.
Pia amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Halmashauri zote nchini zifuatilie watu binafsi, kampuni na viwanda kuhakikisha kuwa sheria na kanuni za udhibiti wa taka hatarishi zinazingatiwa ipasavyo hali ambayo itachangia katika udhibiti wa uchafuzi wa mazingira.
Simbachawene amesema hayo leo ofisini kwake jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu kanuni za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi za mwaka 2019, kanuni za udhibiti na usimamizi wa taka za kielektroniki za mwaka 2019 na kanuni za ada na tozo za usimamizi wa mazingira za mwaka 2019.
Alisema hatua iliyochukuliwa na Ofisi hiyo ya kufanya marekebisho katika kanuni hizi na kuweka mfumo bora wa kisheria wa kusimamia taka hatarishi inalenga sio tu kuhakikisha kuwa mazingira yanalindwa na kusimamiwa bali pia miundombinu ya nchi inalindwa ipasavyo.
“Kama tunavyofahamu, mojawapo ya taka hatarishi ni chuma chakavu, kuna baadhi ya wafanyabiashara na watu ambao sio waaminifu wanafanya biashara hii bila kuwa na vibali husika, lakini pia wapo ambao wana vibali lakini hawafuati masharti yaliyowekwa chini ya vibali hivyo,” alisisitiza.
Aidha waziri huyo aliwataka baadhi ya wanaofanya biashara hiyo huku wakikwepa kulipa kodi stahiki kuacha udanganyifu huo kwani sasa Serikali imeweka mfumo wa kiutawala, kisheria na kikanuni ambao sio rahisi kufanya udanganyifu huo tena bila kugundulika.
Aliongeza kuwa katika kuboresha usimamizi wa mazingira, Ofisi imefanya marekebisho ya Kanuni mbalimbali pamoja na kutunga Kanuni Mpya zikiwemo za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za mwaka 2009.
Kanuni zingine ni za Ada na Tozo za Usimamizi wa Mazingira za Mwaka 2008 na marekebisho yake ya mwaka 2016 na 2018, pamoja na Kuandaa Kanuni mpya za Udhibiti na Usimamizi wa Taka za Kielektroniki za Mwaka 2019.
Simbachawene alifafanua kanuni mpya za mwaka 2019, zimeainisha aina ya shughuli za usimamizi wa taka hatarishi ambazo zinapaswa kuwa na kibali cha Waziri mwenye dhamana ya Mazingira akitaja shughuli zinazopaswa kuombewa kibali ndani ya nchi ni kukusanya, kutunza, kusafirisha na kumiliki au kuendesha mtambo wa usimamizi wa taka hatarishi.
Aidha, shughuli za usafirishaji nje ya nchi, kuingiza au kupitisha nchini taka hatarishi zinapaswa kuombewa kibali ambacho pia hutolewa na Waziri husika na zimeelekeza shehena yoyote ya taka hatarishi itakayoingizwa au kupitishwa nchini bila kufuata masharti ya Kanuni hizi, itachukuliwa kuwa ni usafirishaji haramu wa taka hatarishi na zinapaswa kurejeshwa katika nchi zilikotoka kwa gharama za msafirishaji.
Waziri Simbachawene aliongeza kuwa kanuni hizi zimeweka adhabu kali zaidi kwa makosa ya kutokuwa na kibali cha kusimamia taka hatarishi nchini zikiwemo faini kuanzia sh. milioni tano hadi bilioni 10 au kifungo kisichozidi miaka 12 au vyote kwa pamoja.
“Napenda kusisitiza kuwa hatua hii iliyochukuliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ya kufanya marekebisho katika Kanuni hizi na kuweka mfumo bora wa kisheria wa kusimamia taka hatarishi inalenga sio tu kuhakikisha kuwa mazingira yanalindwa na kusimamiwa bali pia miundombinu ya nchi inalindwa ipasavyo.
“Kama tunavyofahamu, mojawapo ya taka hatarishi ni chuma chakavu, kuna baadhi ya wafanyabiashara na watu ambao sio waaminifu wanafanya biashara hii bila kuwa na vibali husika, lakini pia wapo ambao wana vibali lakini hawafuati masharti yaliyowekwa chini ya vibali hivyo. Moja ya sharti muhimu ni kwamba kila mwenye kibali cha chuma chakavu anapaswa kutoa taarifa ya chanzo cha chuma chakavu hicho na mahali anapokipeleka. Na hiyo inafanyika kwa kujaza ‘tracking form’ namba 3, kutokufanya hivyo ni kosa kubwa chini ya Kanuni hizi,” alitahadhatrisha.