Home Mchanganyiko VIJANA OPARESHENI MAGUFULI WAPATA NEEMA YA AJIRA

VIJANA OPARESHENI MAGUFULI WAPATA NEEMA YA AJIRA

0

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo kuhusu ajira kwa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa “Operesheni Magufuli” na masuala mbalimbali ya kiutumishi. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael.

Na.Alex Sonna,Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameelekeza vijana wote wenye elimu ya Shahada ya Kwanza waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) “Operesheni Magufuli”  kupewa ajira katika taasisi mbalimbali za serikali.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake eneo la Mtumba jijini Dodoma leo.

“Serikali imekuwa ikiwajengea vijana uadilifu, umoja, mshikamano, moyo wa kujitolea, moyo wa uzalendo, nidhamu na ari ya kupenda kufanya kazi kwa kuwaingiza kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenda Taifa, hivyo kwa kutambua mchango wao, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  ameagiza wapewe ajira’’ Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Dkt. Ndumbaro ametaja sifa za vijana waliohitimu JKT kuwa ni lazima wawe wametumikia kwa kipindi kisichopungua miaka miwili na kwamba wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao binafsi, vyeti vya elimu, taaluma na vyeti vya kuhitimu mafunzo ya JKT katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia barua pepe ya [email protected].

Aidha, Dkt. Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuwaasa waajiri wanaowarejesha makazini watumishi wa umma walioghushi vyeti vya elimu na taaluma kwa visingizio kwamba waliondolewa kimakosa au waliajiriwa kabla ya tarehe 20 Mei, 2001 kwa sifa ya Elimu ya Darasa la Saba.

“Serikali haitosita kumchukulia hatua mwajiri yeyote atakayekiuka maelekezo halali yaliyotolewa na Serikali kuhusiana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi walioghushi vyeti” Dkt. Ndumbaro amesema.

Akizungumzia suala la udanganyifu na upendeleo katika upandishwaji vyeo, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa ofisi yake imebaini baadhi ya waajiri kuwasilisha taarifa za uongo Ofisi ya Rais-Utumishi ili kuwapandisha vyeo watumishi kwa lengo la kuwanufaisha baadhi yao bila kuwa na vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zinazosimamia Utumishi wa Umma.

“Ofisi yangu itaendelea kuwachukulia hatua stahiki waajiri watakaobainika kufanya udanganyifu kwa madhumuni ya kuipotosha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili iweze kutoa vibali vya kuwapandisha vyeo watumishi isivyostahili” Dkt. Ndumbaro amefafanua.

Dkt. Ndumbaro amehitimisha mkutano huo kwa kuwataka Maafisa Utumishi nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma badala ya kuwa chanzo cha kero na matatizo ya kiutumishi.

Mkutano kati ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro na waandishi wa habari ulikuwa na lengo la kuuhabarisha umma juu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi.