Home Mchanganyiko TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA YASHIRIKISHA WADAU MABORESHO YA SERA

TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA YASHIRIKISHA WADAU MABORESHO YA SERA

0


Mkurugenzi
wa Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Bw. Buji Bampebuye akifungua kikao cha wadau wa Ushirika katika kikao
kazi cha kukusanya maoni ya maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika
mkoani Dar es salaam, kulia ni Mrajis Msaidizi wa
Mkoa wa Dar es salaam Bw. Abdillahi Mutabazi
Wadau
wa Ushirika wakijadiliana kuhusu masuala ya kufanyiwa maboresho katika
Sera ya Maendeleo ya Ushirika, mkoani Dar es salaam hivi karibuni
Mrajis
Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara akifungua kikao kazi cha mjadiliano na
kupokea maoni ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika Mkoani Mtwara
Wadau Mkoani Mtwara wakijadiliana maboresho ya kufanyika katika Sera ya Maendeleo ya Ushirika

Mkurugenzi
wa Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Bw. Buji Bampebuye ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Ushirika kutoa
maoni yatakayotumika katika kuboresha na kupitia upya Sera ya Maendeleo
ya Ushirika ya mwaka 2002.

Wito huo umetolewa wakati wa
ukusanyaji wa maoni hayo katika kikao kazi kilichofanyika Dar es salam
hivi karibuni, Tume ilipokutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika pamoja
na wanaushirika waliokuwa wakijadili masuala mbalimbali ya namna bora
ya kuboresha utendaji na uendeshaji wa Sekta ya Ushirika nchini.

“Wanaushirika
tujadiliane kwa kina changamoto zilizopo katika Sekta tutoe mapendekezo
nini kifanyike na namna gani kifanyike ili kuimarisha na kuondokana na
changamoto pamoja na vikwazo vilivyopo katika Sekta ya Ushirika
inayochangia Uchumi wa nchi na kutoa fursa za ajira nchini. Ushirika ni
wa wanaushirika wenyewe kwa hiyo tumieni fursa hizi vizuri kuleta
mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa Taifa letu,” alisema Bw. Bampebuye

Sambamba
na kikao kazi hicho Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara Bw. Juma Mokili
akifungua kikao cha wadau katika ukusanyaji wa maoni mkoani Mtwara
alisema Sera inatoa Dira ya uendeshaji wa Sekta ya Ushirika. Hivyo,
wadau wana mchango muhimu katika kuujenga Ushirika watumie fursa hiyo
kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru ili kuweka msingi wa Sera bora
itakayotumika kuendelea kuunda Sheria, Miongozo pamoja na Kanuni
zitakazotumika kwa maslahi ya wanaushirika na Taifa kwa ujumla.

Pamoja
na mambo mambo mengine wadau walijadili masuala mbalimbali ikiwemo
muundo wa Ushirika, fedha, Uwekezaji katika Vyama, Usimamizi na
Uendeshaji wa miradi ya Pamoja, mali za Ushirika, ubunifu na
Ujasiriamali katika Ushirika, masoko ya bidhaa, huduma za Ushirika,
utawala, usimamizi, utafiti, elimu pamoja na mafunzo ya Ushirika.

Kwa
upande wake Mjumbe wa kikao kazi Mkoani Mtwara Bw.Issa Mangochi kutoka
Chama Kikuu cha Ushirika Masasi na Mtwara (MAMCU) amepongeza utaratibu
huo shirikishi ambao umetoa fursa kwa wadau kutoa maoni na mapendekezo
yao yatakayosaidia kutengeneza Sera bora zaidi itakayo hudumia
wanaushirika wengi zaidi na utendaji wenye tija na maendeleo kwa
wananchi. Aliongeza kwa kuwaomba watendaji katika Sekta ya Ushirika
kufanya kazi zao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia taratibu za
kazi.

Vikao kazi hivyo vimehusisha wadau kutoka maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Vyama vya Msingi (AMCOS), Vyama vikuu,
Taasisi za Vyuo vikuu, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo, Shirika la
Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO). Tume tayari
imeshapokea maoni kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo
Kilimanjaro, Kanda ya Juu Kusini mkoani Mbeya pamoja na Kanda ya Ziwa
mkoani Mwanza.