Na Catherine Sungura,Dodoma
WATANZANIA hususan wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wamehimizwa kuzingatia kanuni za afya na usafi wa mazingira hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua za masika ili kuepuka magonjwa mbalimbali ya ya mlipuko.
Wito huo umetolewa mapema leo na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Leonard Subi.
“Natoa wito kwa watanzania, sasa hivi ni kipindi cha masika, mvua nyingi zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, mvua kubwa ni neema lakini wakati mwingine inaweza kuwa tatizo katika suala la afya ya binadamu.
“Tunakuwa na maji mengi, tunakuwa na mafuriko, kwa hiyo tuendelee kuzingatia kanuni za afya katika maeneo yetu,” amesema Dk. Subi.
Akitoa mfano amesema Jiji la Dar es Salaam lilikumbwa na mlipuko wa homa ya dengue, Serikali ya awamu ya tano imeweza kuudhibiti kwa nguvu zote.
“Tulitumia nguvu zetu zote kuudhibiti, baada ya mvua hizi za masika, hivyo, tuwaombe wakazi wa Dar es Salaam waendelee kuhakikisha wanazingatia kanuni za afya,” amesema.
Dk. Subi ameongeza “Mahala ambapo umezungukwa na maji waendelee kutumia dawa, tulale kwenye vyandarua, fukieni madimbwi na kuondoa vifuu vya nazi, wasiruhusu kuwepo mazalia ya mbu.
“Jambo jingine wasitiririshe vinyesi, wapo baadhi ya wananchi wenye tabia mbaya, wakiona wingu, ikinyesha tu mvua, wanatapisha vyoo, hii ni tabia mbaya, tabia ya uuaji.
“Tunaomba sheria, ichukue mkondo wake, yeyote anayefanya hivyo amevunja sheria ni sawa na anamuambia fulani nenda kafe maana umetumia kinyesi changu,” ametoa rai.
Amewahimizwa kuendelea kuchemsha maji kwa sababu katika kipindi cha msimu wa mvua kama hiki baadhi ya vyanzo vya maji huwa vinachafuliwa.
“Hivyo pamoja na kwamba upatikanaji wa maji katika jiji la Dar es Salaam umeimarika hadi kufikia asilimia 85 bado kuna ile asilimia 15.
“Waendelee kuhakikisha wanatumia maji safi na salama, wachemshe maji ya kunywa, wakiona hawawezi basi watumie dawa ya chlorine, tunayo water guard ambayo ni dawa nzuri katika maeneo yetu,” ametoa rai
Sambamba na hilo, Dk. Subi amehimiza pia kuzingatia unawaji wa mikono hasa kabla ya kula chakula.
“Hizi ni baadhi ya kanuni za afya ambazo tunahimiza wananchi waendelee kuzizingatia, tuna uwezo kabisa wa kupambana na maradhi.
“Tumetolewa pia wito kama unakaa kwenye mabonde hama, Serikali imetoa wito kwa wananchi wote, wale ambao wanakaa kwenye maeneo hatarishi kuhama, kwa sababu ni hatarishi kwa afya lakini pia ni hatarishi kwa maisha yao na familia zao,” amesema.
“Tuwalinde watoto, walemavu na wagonjwa ambayo wanataabika, suala la usafi wa ndani ya nyumba, puliza dawa za mbu ili kujikinga.