Na. Edward Kondela
Serikali imesema imelenga kuimarisha tasnia ya maziwa nchini ili kuongeza uzalishaji na kuleta tija kwa wazalishaji na walaji.
Akizungumza jana (18.12.2019) wakati wa tamasha la vijana katika tasnia ya maziwa Mkoani Kilimanjaro lililoratibiwa na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) pamoja na washirika wengine zikiwemo Halmashauri za Wilaya za Siha na Hai, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ametaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika tasnia ya maziwa nchini kwa kuondoa tozo mbalimbali katika tasnia hiyo.
Naibu Waziri Ulega amebainisha tozo hizo zikiwemo za vibali vya vyombo vya kusafirishia maziwa chini ya lita 51, usajili wa vituo vya kukusanyia maziwa chini ya lita 201, usajili wa wazalishaji wa maziwa chini ya lita 51 na usajili wa wasambazaji wa pembejeo za maziwa.
Aidha amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga kuboresha kosaafu kwa kutekeleza mkakati wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2018/2019 hadi 2020/2021 unaolenga kuzalisha mitamba milioni moja kwa mwaka kutokana na kuzalisha ng’ombe wa asili milioni tatu ili kuongeza uzalishaji wa maziwa.
“Serikali tutaimarisha pia mashamba ya serikali kwa kuyapatia mifugo bora ambayo itasambazwa kwa wafugaji pamoja na kuhamasisha sekta binafsi kuboresha kosaafu za ng’ombe wa maziwa, hivyo wananchi tumieni Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) ili mpate ng’ombe bora na kisasa wa maziwa.” Amesema Mhe. Ulega
Naibu waziri huyo pia amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kudhibiti magonjwa kwa kutumia chanjo zinazozalishwa nchini, kuendeleza kampeni ya uogeshaji mifugo ambapo serikali inatoa ruzuku pamoja na kuboresha sheria za mifugo kwa lengo la kulinda afya na malisho ya mifugo.
Mhe. Ulega ametaja mikakati mingine ya kuimarisha tasnia ya maziwa nchini ikiwemo ya kutoa elimu ya ufugaji bora na kuimarisha tafiti katika tasnia ya maziwa, kuboresha masoko na kuhimiza usindikaji wa maziwa kwa kujenga viwanda pamoja na kuchochea matumizi ya teknolojia sahihi za mifugo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti Mtandao wa Vijana kutoka Wilaya za Siha na Hai Mkoani Kilimanjaro Bi. Regina Urassa ambao wanawezeshwa na miradi ya SNV katika biashara ya mnyororo wa thamani wa maziwa akisoma risala ya vijana hao, amemuomba Naibu Waziri Ulega kuwaunganisha vijana na fursa za kirasilimali na utaalamu pake anapoona inawafaa.
Bi. Urassa ametaja changamoto wanazokabiliana nazo kutofikia malengo yao kwa urahisi zikiwemo za vijana kukosa ardhi kwa ajili ya kufanya shughuli zao kama vile kulima nyasi kwa ajili ya malisho, uhaba wa mitaji ya kutosha kwa ajili ya kuboresha na kupanua biashara zao pamoja na kukumbana na wachuuzi holela wa maziwa ambao wananunua maziwa bila kuzingatia ubora wa maziwa na kupandisha bei kwa sababu hawazingatii ubora, pia kuongeza maji kwenye maziwa ili kufidia bei waliyonunua.
Ameongeza kuwa mahusiano yao ya kibiashara na vyama vya ushirika bado hayajawa imara kiasi cha kuweza kutumia mifumo ya vyama vya ushirika kuwafikia wafugaji ambao ni wateja wao.
Amefafanua kuwa vijana hao wa Wilaya za Siha na Hai walihamashishwa na mradi wa mnyororo wa thamani wa maziwa unaoratibiwa na SNV pamoja na washirika wengine zikiwemo Halmashauri za Wilaya za Siha na Hai ambapo kuna vikundi 19 vya vijana vyenye jumla ya vijana 747 ambapo wamepatiwa mafunzo na vitendea kazi.
Katika hatua nyingine mgeni rasmi naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa katika tamasha la vijana katika tasnia ya maziwa Mkoani Kilimanjaro ametembelea mabanda ya wadau wa maziwa yaliyokuwa yameandaliwa ili kujionea shughuli mbalimbali wanazofanya.
Aidha Mhe. Ulega amepata fursa ya kutembelea kijiji cha Mwangaza kilichopo Wilaya ya Siha na kujionea kikundi cha vijana wanaolima malisho ya mifugo na kuahidi kutoa mchango wa Shilingi Milioni Moja ili kuwawezesha vijana hao waweze kujiendeleza zaidi.
Mhe. Ulega amefika pia katika Wilaya ya Hai na kujionea utendaji kazi wa mashine ya kisasa ya kuuzia maziwa pamoja na kiwanda cha kuzalisha maziwa cha Nronga.