Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Afya na Taasisi zake wakiwa pamoja na Waandishi wa Habari walipotembelea Maabara ya NIMR Mkoani Mbeya.
Mtaalamu wa Maabara Abisai Kisinda akionesha mtungi wa Liquid Nitrogen Tank wa kuvuna Nitrogen kwa ajili ya kuhifadhia sampuli za utafiti ulioko kwenye maabara ya NIMR mkoani Mbeya.
Mtaalamu wa Maabara Bariki Mtafya akionesha mashine za Gene Xpert zinazotumika kupima sampuli za Kifua Kikuu zilizoko katika Maabara ya NIMR Mkoani Mbeya.
Mkurugenzi wa NIMR Mkoani Mbeya, Dkt. Nyanda Ntinginya akiongea na maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara ya Afya na Taasisi zake ambao wametembelea nyanda za juu kusini katika kutekeleza kampeni ya “Tumeboresha Sekta ya Afya”.
…………………………………………..
Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu kanda ya nyanda za juu kusini (NIMR) imepiga hatua kubwa katika shughuli za utafiti inazofanya ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa vya maabara pamoja na watalaamu waliobobea.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa NIMR wa kanda hiyo Dkt. Nyanda Ntinginya wakati akiongea na maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara ya Afya na Taasisi zake ambao wametembelea nyanda za juu kusini katika kutekeleza kampeni ya “Tumeboresha Sekta ya Afya” ili kuona mafanikio ya sekta ya afya katika kipindi cha miaka mitano ya Rais John Magufuli akiwa madarakani.
Dkt. Nyanda amesema moja ya mafanikio makubwa ya NIMR ya kanda hiyo ni Utafiti wa vipimo vya awali vya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa watoto wachanga waliozaliwa na akina mama wenye maambukizi.
Utafiti huo ujulikanao kwa jina la ‘BABY’ uliofanywa na Taasisi hiyo unatumia kipimo cha “Early Infant Diagnosis (EID)” ambacho ufanyika kwa kutumia mashine za Gene Xpert.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyanda amesema awali, upimaji wa kawaida ulikuwa unafanywa kwa watoto wachanga wenye wiki 4 hadi 6 na majibu yake yalikuwa yakichukua wiki mbili.
Dkt. Nyanda amesema utafiti huo uliofanyika Julai 2015 hadi Novemba 2016 kituo cha NIMR Mbeya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Munich cha nchini Ujerumani ulilenga kutathimini vipimo vya awali vya VVU kwa watoto wachanga ambao wazazi wao wameathirika.
“Huu utafiti ulilenga kufanya tathmini ya vipimo vya awali vya VVU katika kituo cha kutolea huduma na vipimo vilifanywa na wauguzi tofauti na upimaji wa sasa ambao huhitaji wataalamu wa maabara na hivyo kuhitaji usafirishaji wa sampuli za damu kwenda maabara ya kanda au ya mkoa”. Amesema Dkt. Nyanda.
Matokeo ya utafiti yameonesha vipimo hivyo vilifanya vizuri kwa asilimia 100 na vinatoa majibu ndani ya masaa mawili tu na hivyo mgonjwa kupewa majibu yake siku hiyo hiyo ukilinganisha na upimaji wa kawaida ambapo huchukua wiki mbili au zaidi kupata majibu.
“Upimaji wa VVU wa awali kwa watoto wachanga umejumuishwa katika muongozo wa sasa wa utoaji wa huduma za VVU nchini,”alisema.
Hata hivyo, matokeo ya utafiti huo uliofanywa nchini Tanzania, Afrika ya kusini na Msumbiji yamepelekwa Shirika la Afya Duniani(WHO) kutoa miongozo ya upimaji wa VVU kwa watoto hao katika muongozo wa utoaji wa huduma za VVU wa mwaka 2016.
Maabara ya Taasisi ya Taifa ya utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ya Mkoani Mbeya imepata ithibati ya ubora wa kimataifa Maabara za utafiti ya nchini Marekani “College of American Pathologists” (CAP) kutokana na ubora wake wa kufanya tafiti ambapo ithibati hiyo imetolewa kwa nchi mbili tu katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa ni Tanzania na Uganda.