Na Innocent Natai, TPRI, Arusha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe ameshangazwa na kuwepo kwa baadhi ya halmashauri zinazotoza ushuru wa mazao ya mbegu,kitendo ambacho ni kinyume na maelekezo ya serikali na kinarudisha nyuma jitihada za serikali za kuhakikisha nchi inaongeza uzalishaji wa mbegu na kuacha kununua mbegu kutoka nje ya nchi.
Mtigumwe ameyasema hayo tarehe 17 Disemba 2019 wakati wa kikao cha utekelezaji wa tasnia ya mbegu hapa Nchini, ikiwemo kupitisha aina mpya za mbegu bora za mazao, kupitia changamoto za uzalishaji wa mbegu hapa nchini, Kilicho jumuisha ujumbe kutoka TARI (Tanzania Agricultural Research Institute), Ofisi ya hatimiliki za wagunduzi wa mbegu, Idara ya mazao, na Taasisi ya udhibiti ubora wa mbegu (TOSCI).
Wengine ni Chama cha Wafanyabiashara wa Mbegu Tanzania, Mwakilishi kutoka Vyuo vikuu vya Kilimo, Maendeleo ya Mazao, Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), na Wakala wa mbegu za kilimo (ASA) uliofanyikia katika ukumbi wa mikutano TPRI Makao Makuu Arusha.
Amesema halmashauri kutoza ushuru kwenye mazao ya mbegu ni kosa kwani maelekezo ya serikali kuhusu suala hilo yalishatolewa na mbegu za kilimo ni tofauti na mzao ya chakula na biashara yanayo zalishwa, hivyo kufanya hivyo kunakwamisha adhma ya serikali ya kuhakikisha uzalishaji wa mbegu unaongezeka na taifa kuacha kununua mbegu kutoka nje.
Amesema serikali imejipanga kuhakikisha suala hilo linafanikiwa kwa kipindi kifupi ikiwemo kuwaondolea vikwazo wazalishaji wa mbegu na kuwatatulia kero mbalimbali zinazowafanya washindwe kuzalisha kwa wingi na kuwataka wazalishaji wa mbegu kutoa nje kufanyia uzalishaji wa mbegu zao hapa nchini na kuacha ule utaratibu wa awali wa kuzalishia nje na kuja kuuza hapa nchini.
Aidha, amezitaka taasisi zote zinazohusiana na tasnia ya Mbegu kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ili kusaidia mkakati wa kitaifa wa uzalishaji mbegu unatimia ikiwemo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakulima ya kutambua mbegu bora,mbegu zisizo bora,kanuni za mbegu bora ikiwemo kuacha kurudia mbegu kwa muda mrefu.
Ameitaka Taasisi ya Kudhiti Ubora wa Mbegu (TOSC) kuhakikisha inaongeza kasi ya ukaguzi na kubaini wauzaji na wasambazaji wa mbegu zisizo bora na feki au bandia na watakao bainika kuchukuliwa hatua ili kuwahakikishi wakulima usalama wa kilimo chao na kufanya tasnia ya kukua na taifa kujitosheleza kwa mbegu zilizo bora.
Kakao hicho kimeazimia kwa pamoja kupitisha aina mpya za mbegu bora za mazao takribani 40 ambazo ni za mazao ya Mahindi aina 10, Mpunga aina 2, Ulezi aina 1, Pamba aina 3, Mhogo aina 9, Alizeti aina 9 na Viazi vitamu aina 6.