*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mashirika mbalimbali yanayojihusisha na kulinda na kutetea haki ya mtoto wa kike nchini wakiwemo viongozi wa madhehebu mbalimbali wamekutana kwa pamoja na kujadili ni namna gani wanaweza kutokomeza tatizo la ndoa za utotoni.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Save the Children Bw.Peter Walsh amesema kuwa kitendo cha kukutana na wadau mbalimbali kujadili ni namna gani wanaweza kuondoa tatizo hilo wanaamini kufikia mwaka 2020 tatizo hilo litakuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.
“Suala zima la ndoa za utotoni linaanzia katika familia kuna mila na desturi zenu ambazo zimekuwa zikiendelea kuendekeza suala hili kuna baadhi ya maeneo tatizo hili limekithiri kwa kiasi kikubwa na ndo maana leo tumekutana na kulijadili suala hili”. Amesema Bw.Walsh.
Aidha, Bw, Walsh amesema kupitia marekebisho ya sheria ya ndoa za utotoni na kuruhusu mtoto kuolewa akiwa na umri kuanzia miaka 18 kutachangia kuondokana na tatizo la ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2020.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bright Jamii Initiative, Bi.Irene Fugara amesema wamekutana kwa pamoja na kuangalia ni namna gani wanaweza kulisimamia tatizo hilo na kuweza kulimaliza.
Aidha, Bi.Irene amesema kuwa pamoja na baadhi ya jamii wanafahamu madhara ya ndoa za utotoni kuna wengine bado wanaendelea vitendo hivyo kutokana na mila na desturi pamoja na imani zao.
“Bado muendelezo wa ndoa za utotoni unaendelea kuwepo kasababu unakuta jamii bado inamtazamo fulani kuhusiana na masuala ya mtoto wa kike, tafiti ambazo tumekuwa tukizifanya kama wanachama wa mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni zinaonesha kwamba kuna jamii nyingi ambazo zinamuona mtoto wa kike kama si mtu wa muhimu na kumpa kipaumbele kama mwanajamii ambaye anaweza kuchangia maendeleo ya taifa”.Amesema Bi.Irene.
Nae Mkurugenzi wa miradi wa Plan international Bw. Peter Mwakabwale amesema kuwa wamekuwa wakiwaelimisha jamii ujumla kupitia madhehebu mbalimbali wakiwemo wakristo na waislamu pamoja na kuwatumia watu mashuhuli ambao inakuwa rahisi sana kuelimisha jamii na kuhakikisha ndoa za utotoni zinapungua kwa kiasi kikubwa.
“Tunafurahia kuona Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 imekubaliwa kuweza kurekebishwa na kuweza kuruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa kuanzia miaka 18 kwasababu takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa asilimia 59 ukifuatiwa na mkoa wa Tabora kwa asilimia 57, kwa hali kama hii tutakuwa na watoto wakilea watoto katika mikoa hii miwili”. amesema Bw.Mwakabwale.
Hata hivyo kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti la Katiba na Sheria Mh.Mohammed Mchengelwa amesema kuwa ipo haja ya jamii kuelewa misingi imara ya karne tulionayo ambayo ni ulinzi kwa watoto wetu na wao kama wabunge wamekuwa wakiipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa ulinzi kwa watoto.