Home Mchanganyiko Waziri Mhagama aridhishwa na utendaji wa OSHA

Waziri Mhagama aridhishwa na utendaji wa OSHA

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwahutubia watumishi wa OSHA katika kikao chao cha tatu cha baraza la tano la wafanyakazi (hawako pichani) jijini Dodoma jana. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda. Watatu na nne kutoka kulia ni viongozi wa Tughe Taifa na ngazi ya tawi. Baadhi ya wafanyakazi wa OSHA wakifuatilia hotuba ya Mgeni Rasmi, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) katika kikao chao cha tatu cha baraza la tano la wafanyakazi jijini Dodoma
jana.

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ameeleza kuridhishwa kwake na utendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambapo amesema taasisi hiyo ya serikali imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

 

Waziri alitoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya OSHA katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020 iliyowasilishwa mbele yake na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija
Mwenda, katika kikao cha tano cha Baraza la tatu la Wafanyakazi wa taasisi hiyo ambacho kilifunguliwa na Waziri Mhagama jana jijini Dodoma.

 

“Niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kuhakikisha kuwa afya za wafanyakazi ambao ndio wanaosaidia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa hili zinazingatiwa katika maeneo yao ya kazi”. Alisema Mhagama.

 

Katika taarifa yake aliyoiwasilisha mbele ya Waziri, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA ameainisha mafanikio ya kiutendaji ambayo taasisi yake imeyapata katika nusu ya mwaka wa fedha 2019/2020.

 

“Mhe. Waziri katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba mwaka huu tumepata mafanikio makubwa sana katika utekelezaji wa majukumu yetu. Tumesajili maeneo ya kazi 1,919 kati ya 2,324 yaliyopangwa, tumefanya ukaguzi katika maeneo ya kazi 8,234 kati ya 10,000 yaliyokuwa
yamepangwa”.Aliainisha Kiongozi huyo wa OSHA katika taarifa yake.

 

Mafanikio mengine yaliyoelezwa na Mtendaji wa OSHA ni pamoja na; Kupima afya kwa wafanyakazi 90,193 zaidi ya idadi ya wafanyakazi 75,032 iliyokuwa imepangwa, kutoa adhabu kwa waajiri 80 ambao walishindwa kukidhi vigezo vya afya na usalama katika maeneo yao ya kazi na kuandaa kanuni saba (7) ambazo zipo katika hatua mbali mbali za utungwaji.

 

Aidha, Waziri Mhagama aliwataka OSHA kuongeza juhudi zaidi katika utendaji ikiwemo kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi maambukizi ya UKIMWI katika maeneo ya kazi ambapo alisema pamoja na takwimu kuonyesha kwamba maambukizi yanapungua kitaifa, changamoto hiyo bado inaendelea kuwakumba watanzania hasa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24.

 

OSHA ni taasisi ya serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo husimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Jukumu kuu la OSHA chini ya Sheria tajwa na kusimamia viwango
vya usalama na afya katika sehemu za kazi ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kuwasababishia ajali na magonjwa wanapokuwa
kazini.