Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyasosi wilayani Bariadi kabla ya kuwasha umeme katika eneo hilo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( mwenye shati la bluu) akisalimiana na watumishi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufika katika uzinduzi wa Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme kilichopo eneo la Ng’ami wilayani Bariadi mkoani humo.
Eneo la Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme kilichopo katika eneo la Ng’ami wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata utepe kuashiria kuwasha kwa umeme katika kijiji cha Nyasosi wilayani Bariadi mkoani Simiyu. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.
***********************************
Hafsa Omar – Simiyu
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amezindua Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia Kuu za Umeme (Switching Station) kilichopo katika kijiji cha Ng’ami, eneo la Viwandani, wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.
Uzinduzi huo umefanyika Desemba 15, 2019 ambapo Kituo hicho kinachukua umeme kutoka Kituo Kikuu cha Mabuki kilichopo Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza umbali wa kilomita 87.2, kupitia Njia ya kusafiri umeme ya Msongo wa kV 33.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya uzinduzi huo, Dkt Kalemani, alisema kituo hicho kimezinduliwa rasmi kwa lengo la kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika Mkoa wa Simiyu ambao umejikita katika uwekezaji wa Viwanda , na hivyo unahitaji umeme wa uhakika.
Kutokana na uwepo wa Kituo hicho, Dkt. Kalemani alisema “natoa agizo kwa Meneja wa Mkoa, mtafute eneo la kiwanja hapa, mjenge eneo la makazi kwa ajili ya mtumishi atakayekiangalia kituo hiki kwa masaa 24, kwa sababu ikitokea dharura haitowezekana mtu kutembea kilomita 10 kuja hapa hivyo ni lazima mtu akae hapa.”
Aidha, Dkt Kalemani alitoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, kuwahamasisha wananchi wa eneo hilo kutunza miundombinu ya kituo husika ili wananchi wasifanye uharibu wa aina yoyote katika eneo hilo, ambalo ni muhimu kwenye maendeleo ya shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Vile vile, alisema ifikapo mwezi Machi mwakani Kituo Kikuu cha Kupoza umeme cha Imalilo kilichopo wilaya ya Bariadi, mkoani humo nacho kitakuwa kimekamilika ambapo kitawezesha wananchi wa Mkoa huo na maeneo ya jirani kupata umeme wa uhakika na wakutosha kwa ajili ya matumiza ya kawaida na Viwanda vilivyopo mkoani humo.
Aidha, alisema kuwa, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa Mkoa huo ambazo zinatumika kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu ya umeme iliyoharibika na kusambazia umeme katika maeneo ambayo bado hayajapata umeme.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka aliishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ili kuhakikisha umeme unapatikana nchi nzima.
Alisema, Mkoa huo unaenda kwenye Mapinduzi ya Viwanda kwa haraka na ujio wa kituo hicho utaharakisha maendeleo ya Viwanda mkoani humo.
Aliongeza kuwa, wawekezaji waliofika mkoani Simiyu walitaka wajenge viwanda karibu na eneo ambalo lipo karibu na kituo hicho cha umeme na Serikali imeridhia ombi hilo.
Katika ziara yake mkoani humo, Waziri wa Nishati, alitembelea eneo kutakapojengwa Kituo cha Kupoza Umeme, Imalilo wilayani Bariadi na kuwasha umeme katika kijiji cha Nyasosi kilichopo wilayani humo.