Na ASP. Lucas Mboje, Dar es Salaam
JUMLA ya Wafungwa 5,533 katika magereza mbalimbali nchini walionufaika na msamaha wa Rais wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wameachiliwa huru magerezani.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike amesema kuwa utekelezaji wa zoezi la kuwaachiliwa huru wafungwa wote walionufaika na msamaha wa Rais umekamilika nchi nzima.
“Ni matarajio yangu kuwa wafungwa walioachiliwa wamejutia makosa yao na wataacha kutenda uhalifu hivyo kujihusisha na shughuli halali kwa maendeleo yao, familia zao, jamii na taifa kwa ujumla”, amesisitiza Jenerali Kasike.
Aidha, Kamishna Jenerali Kasike ameelezea manufaa mbalimbali ya msamaha huo; mosi kupungua kwa msongamano magerezani, pili, wanufaika wa msamaha kujumuika na familia zao, tatu, kichocheo cha urekebishaji magerezani kwani msamaha huo utasaidia kuimarika kwa nidhamu na kurejesha matumaini kwa wanaobakia magerezani pamoja na wanufaika wa wamsamaha huo kupata fursa ya kujishughulisha na shughuli za maendeleo uraiani.
“Zipo changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa zoezi hili ambapo baadhi ya wafungwa walionesha kuwa hawako tayari kuungana na jamii zao pamoja na waliosamehewa kurejea kutenda makosa mara baada ya kuachiwa huru. Hata hivyo nitoe wito kwa jamii nchini kuwapokea wafungwa hao na kuacha kuwanyanyapaa”, amesema Jenerali Kasike.
Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Kasike amemshukru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa msamaha huo ambao ni wa kihistoria hapa nchini. Pia amewapongeza wanahabari wote nchini kwa namna walivyoshiriki kutoa habari za zoezi la msamaha huo katika ngazi ya Mkoa na wilaya.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45(1) (d) imempa mamlaka Rais kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani. Kwa kutumia Ibara hiyo Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru ambapo kilele chake kilifanyika Mkoani Mwanza Desemba 9, 2019.