Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu akihutubia hadhara
iliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya Kenya jana
jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasilisha hotuba yake wakati wa
maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya Kenya yaliyofanyika jana jijini Dar
es Salaam. Kushoto kwake ni Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu akigonga glasi na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) ikiwa ni ishara ya upendo, umoja na mshikamano baina ya nchi
hizo mbili mara baada ya kuzindua rasmi maadhimisho ya miaka 56 ya
Jamhuri ya Kenya jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wageni waalikwa wakiimba nyimbo za taifa za Tanzania pamoja na
ya Kenya kabla ya kuanza rasmi kwa sherehe za maadhimisho ya miaka 56
ya Jamhuri ya nchi hiyo.
Baadhi ya wageni waalikwa wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya
Jamhuri ya Kenya jana jijini Dar es Salaam.
********************************
Tanzania na Kenya zimeahidi kuendeleza na kushirikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.
Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 56 ya Jamhuri ya Kenya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa Tanzania na Kenya ni ndugu na nchi hizo zitaendelea kushikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya diplomasia ya uchumi baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.
“Sisi Tanzania na Kenya ni ndugu wa damu, kwa hiyo basi tunawatakia sana kila la kheri katika kuiletea Kenya maendeleo…lakini mjue kuwa maendeleo ya Kenya ni maendeleo ya pia ya Tanzania, maendeleo pia ya Uganda, ni maendeleo pia Burundi, maendeleo pia Rwanda na Maendeleo pia ya Sudani Kusini na ni
maendeleo pia ya jumuiya ya Afrika Mashariki”. Amesema Prof. Kabudi.
Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu ameishukuru
Serikali ya Tanzania kwa umoja na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa
Kenya na kusema kuwa umoja huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa
Tanzania na Kenya.
“Napenda kuwafahamisha kuwa umoja na mshikamano wetu umekuwa chachu ya maendeleo baina ya mataifa haya mawili…..tukumbuke kuwa umoja ni nguvu na dhamira yetu ni kushirikiana na mataifa yote duniani. Na dhamira yetu ni kuishi kwa amani umoja na mshikamano ili kukuza uchumi wetu”. Alisema Balozi Kazungu.
Aidha, Balozi Kazungu amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa ya kipekee kwa taifa la Kenya kutokana na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa nchi ya Kenya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
“Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili 2019 Kenya tulipokutana na Tanzania jijini
Arusha tuliweza kuondoa vikwazo vya biashara 25 kati ya 37, hii inadhihirisha ni
kwa jinsi gani Kenya na Tanzania na ndugu ambao wanapenda kukuza na
kuendeleza maendeleo ya biashara”. Ameongeza Balozi Kazungu.