NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MBUNGE wa jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara-Kibaha kufikia asilimia 59.1 na kudai kukamilika kwa barabara hiyo kuna kwenda kuinua uchumi wa mji huo na kujibu changamoto ya msongamano wa magari.
Aidha ameomba serikali na taasisi husika kuangalia umuhimu wa ombi lake la kuomba ujenzi wa barabara hiyo awamu ya kwanza ivuke mji wa Kibaha ili kuleta manufaa ya maendeleo ya mji huo unaoelekea kuwa manispaa ,kuliko kuishia mwanzoni mwa Kibaha .
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kutembelea baadhi ya miradi kuonyesha wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ,Kibaha Mjini utekelezaji wa ilani hasa miradi ya kitaifa,kijimbo na kikata,Koka alisema, serikali inafanya kazi kubwa kutatua changamoto za miundombinu ya barabara na sekta nyingine kwa maslahi ya Watanzania.
“Barabara hii inakwenda kupunguza msongamano na kuinua uchumi wa Kibaha”tunashukuru kwa kasi anayokwenda nayo mkandarasi na nimpongeze Rais dokta John Magufuli kwa jitihada zake kuelekeza nchi katika uchumi wa kati”alielezea Koka.
Akitembelea ujenzi wa hospital ya wilaya Lulanzi, kata ya Pichandege ,Koka alisema fedha milioni 220 inayohitajika kukamilisha ujenzi huo itasaidia kuanza kwa huduma haraka hivyo atalisimamia suala hilo.
Wajumbe hao pia walipitia ujenzi wa soko la kisasa ,na mbunge huyo alibainisha litakuwa ni kariakoo ya Kibaha kwani mahitaji yote yatapatikana mjini hapo.
“Tangu jimbo hili lianze ,haijawahi kutokea kuambatana na ujumbe huu mzito, lakini nimesukumwa kutokana na kwamba halmashauri inapokea utekelezaji wa ilani hivyo wamekuja kushuhudia utekelezaji huo ili wakirudi kwa wananchi waweze kueleza serikali inafanya yapi makubwa ,”
Nae mwakilishi wa meneja wa TANROADS Dar es salaam ,ambae ni msimamizi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara-Kibaha ,Issa Mbula alisema ujenzi wa mradi huo,umefikia asilimia 59.1 na muda wa mradi umefikia asilimia 60 na utagharimu sh.bilioni 140 .
Akiongea katika mradi wa ujenzi wa hospital ya wilaya,mganga mkuu wa mji wa Kibaha, Dokta.Tulitweni Mwinuka alisema walipokea serikalini bilioni 1.5 na halmashauri milioni 290 lakini wanahitaji ziada ya milioni 220 ili kukamilisha ujenzi huo.