Waziri wa Madini Doto Biteko akikagua baadhi ya nyaraka za manunuzi ya Madini kwenye moja ya chumba cha kununulia Madini kwenye soko la Maganzo wilaya ya Kishapu.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Mwadui Mhandisi Ayubu Mwenda akitoa maelezo kwa Waziri wa Madini Doto Biteko wakati wa ziara yake mgodini hapo akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack
Waziri wa Madini Doto Biteko akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack muda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao na wafanyakazi wa mgodi wa Mwadui hawapo pichani
Sehemu ya Wananchi wa kijiji cha Maganzo wakimsikiliza . Waziri wa Madini Doto Biteko hayupo pichani wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
…………………
Na Issa Mtuwa – Shinyanga
Uongozi wa Mgodi wa Diamond Williamson (Mwadui) unaozalisha madini ya Almasi uliopo mkoani Shinyanga wilayani Kishapu umeagizwa na kupewa muda wa mwezi mmoja hadi kufikia Januari 2020 kuanza kuuza 5% ya Almasi yote inayozalishwa katika mgodi huo kwenye soko la ndani hususani soko la Kishapu huku wazawa wakipewa fursa ya kununua Almasi hiyo.
Waziri wa Madini Doto Biteko, ameyasema hayo tarehe 10/12/2019 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na uongozi wa mgodi wa Mwadui wakati wa kikao chake alipotembelea mgodini hapo kwa ziara ya kikazi na baadae kuongea na wafaanya biasharaa wa madini wa soko la Kishapu na kisha kuongea na wananchi wa Maganzo wilayani humo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Maganzo.
“Ndugu zangu, nafurahi kuona namna mlivyo kusanyika, bila shaka mnashauku kubwa ya kusikia nikisema jambo. Kabla sijasema naomba niwaambie, Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli amedhamiria kuona maisha ya watu yanabadilika kupitia raslimali za madini hasa wale wanaozungukwa na migodi, wakiwemo ninyi”
“Nataka nione maisha yenu yanabadilika kutokana na uwepo wa mgodi huu na uwepo wa Almasi hii hapa Kishapu. Sasa niseme yafuatayo; Moja, kiliochenu cha muda mrefu cha kuomba mabaki ya mchanga uliochenjuliwa (tellings) nimeagiza kuanzia tarehe 22/12/2019 mchanga ule uanze kutolewa na mkaanze kuufanyia kazi. Pili ifikapo Januari 2020, 5% ya Almasi inayozailishwa mgodini hapa wataanza kuuza kwenye soko la hapa Maganzo na watakao nunua Almasi hiyo ni wazawa wanao nunua kwenye soko la Magazo” aliseema Biteko.
Biteko ameongeza kuwa, kila watu mahali walipo wanufaike na walichopewa na Mungu huku akisema wapo waliopata Bahari, Ziwa, Mbuga za wanyama, Vipepeo, Mijusi, Madini na ninyi wa Kishapu mmepewa Almasi kwa hiyo tumieni uwepo wa Almasi kubadilisha maisha yenu, wizara ya madini itaendelea kusimamia na kuhakikisha fursa zinazotokana na uwepo wa mgodi huu zinawanufaisha
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Diamond Williamson Mhandisi Ayubu Mwenda alisema siku zote wanafanya kazi zao kwa taratibu na kwa kuzingatia sheria. Aliongeza kuwa hawana tatizo na uuzaji wa 5% ya Almasi kwenye Soko la ndani hivyo kama uongozi watatekeleza agizo la Waziri na wataanza kuuza mwezi Januari 2020. Kuhusu utoaji wa mchanga wa “makinikia” utaanza kutolewa tarehe 22/12/2019.
Wananchi wa Maganzo walishukuru kwa ujio wa Waziri wa Madini huku wakifurahishwa na agizo la kuanza kwa tarehe ya utoaji wa mchanga wa makinikia. Zainabu Issa mkazi wa Maganzo alisema mchanga huo wataufanyia kazi na watapata kipato kitakacho wasaidia kuendesha maisha yao huku, Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) Gregory Kibusi alisema wao kama SHIREMA wamefurahishwa na maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Waziri na walikuwa wanayasubiri kwa muda mrefu na watafuatilia.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa soko la Maganzo Seif Khatibu alisema, amefurahishwa na kauli ya waziri kuuagiza mgodi wa Mwadui kuuza 5% ya Almasi yao kwenye soko la Maganzo na inunuliwe na wanunuzi wazawa wa soko la Maganzo.