***********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Baada ya kuoneka vijana wengi kukosa ajira pindi wanapomaliza masomo yao ya elimu ya juu,baadhi ya vijana wa Chuo Kikuu Mlimani wameamua kutengeneza mfumo wa Smart Stock ambao unaweza kumuwezesha mfanyabiashara wa kati na wadogo kurekodi mauzo,manunuzi pamoja na bidhaa alizonazo dukani kwake.
Akizungumza katika Maonesho ya biashara yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Bw.Joshua Mshana amesema kuwa mfumo huo ni bora kwani unaweza kumsaidia mfanyabiashara kurekodi bidhaa na kuweza kufahamu ni bidhaa ipi inauzika kwa haraka ili aweze kufanya manunuzi na wakati gani aweze kununua bidhaa gani.
“Mfumo huu unampa taarifa za kifedha za biashara yake muuzaji ama mfanyabiashara kama anataka kupeleka Benki kwaajili ya mikopo ama anataka kumpatia muwekezaji”.Amesema Bw.Mshana.
Aidha Bw.Mshana amesema kuwa Smart Stock unaweza kutumia kwenye simu ama kwenye kompyuta mpakato kwa gharama ya Tsh.23,000 kwa mwezi.
“Malengo yetu ni kuweza kuwapata wafanyabiashara wadogo na wasaizi ya kati ili waache kutumia makaratasi ambayo ni rahisi kupotea au kuharibika na mvua”. Ameongeza Bw.Mshana.