Mwenyekiti wa Chama cha TACA akiwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho katika kikao na wanahabari kueleza ni namna gani wanaweza kuondoa madalali ambao si rasmi kuona ni namna gani wanaweza kuwasajili madalali ili kuweza kutambulika.
**********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Madalali nchini wametakiwa kujitokeza katika Chama Cha Madalali TACA kwaajili ya kusajiliwa ili waweze kutambuliwa rasmi na kuondokana na utapeli unaoendelea kwa baadhi ya watu wanaojiita madalali.
Ameyasema hayo leo Mwenyekiti wa Chama Cha Madalali Tanzania TACA, Bw.Phidel Katundu katika kikao na Wanahabari katika ofisi ya Chama hicho Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo Bw.Katundu amesema kuwa wanampango wa kuwasajili madalali kwenye chama chao na mwisho watawakagua kila mwaka kwasababu kuna leseni zingine zinakuwa zimefika mwisho.
“Tunampango kila ifikapo mwezi Januari tunamkagua kila mwanachama kuna anavibali vyote ikiwemo kulipa kodi Serikalini ama leseni zinazomruhusu kuwa dalali na tukishajilizisha tunatoa cheti kwenye chama kwa mtu yeyote amtambue na kumpatia ushirikiano”. Amesema Bw.Katundu.
Aidha Bw.Katundu amesema kuwa changamoto kubwa ambayo inawakabili ni kuingiliwa na madalali ambao si rasmi yaani ambao wamekuwa matapeli na kuweza kuchafua sifa ya mwanachama wa TACA.