Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( mwenye kilemba) akiangalia kazi
ujenzi wa msingi wa kusimika nguzo kubwa ya umeme wa kV 220
utakaotumika katika reli ya kisasa, unayoendelea katika njia ya kusafirisha
umeme.
Muonekano wa Moja ya nguzo kubwa ya umeme wa kV 220 baada ya
kusimamishwa tayari kwa kupitisha nyaya.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akitoa maelekezo kwa wasimamizi
wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa utakaotumika katika reli ya kisasa baada ya kutembelea na kukagua ghala la kuhifadhia vifaa hivyo
lililopo Kibaha, mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na baadhi ya
wafanyakazi/ vibarua katika ghala la kuhifadhi vifaa vya ujenzi wa njia ya
kusafirisha umeme mkubwa utakaotumika katika reli ya kisasa, lililopo
Kibaha, mkaoani Pwani.
Baadhi ya vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme
mkubwa utakaotumika katika reli ya kisasa vilivyohifadhiwa katika ghala
lililopo kibaha mkoani Pwani.
*********************************
Na Zuena Msuya, Dar es salaam
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema ameridhishwa na ujenzi
wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme wa kV 220 inayoendelea
kujengwa katika Reli ya kisasa kutoka jijini Dar es salaam hadi mkoani
Morogoro .
Mgalu alieleza hayo Desemba 7,2019 baada ya kufanya ziara ya kukagua
maendeleo ujenzi wa miundombinu hiyo kuanzia Kituo cha Kinyerenzi,
Pugu hadi Kisarawe jijini Dar es salaam ambapo asilimia 70 ya kazi hiyo
imekamilika.
Alitumia ziara hiyo kuwathibitishia watanzania kuwa mradi huo wa ujenzi
wa njia ya umeme utakamilika kwa wakati kulinga na makubaliano ya
mkataba na umeme upo mwingi na wa kutosha kuwezesha reli hiyo
kufanya kazi yake wakati wote.
Alifafanua kuwa ujenzi wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme
inatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2020 ili kutoa fursa ya kuanza
majaribio ya safari kwa kutumia Treni ya umeme, kabla ya kuanza rasmi
kwa safari hizo mwezi Julai, 2020.
“Niwatoe hofu wale wote wenye mashaka na usafiri wa reli kwa kutumia
umeme, umeme upo mwingi na wa kutosha nchini, kwa sasa tunazalisha
zaidi ya megawati 1601, tunazotumia ni megawati 1116 tu, pia kazi ya
kujenga miradi mikubwa ya kuzalisha umeme mwingi zaidi inaendelea,
ukiwemo Mradi wa Julias Nyerere katika bonde la mto Rufiji, Rusumo na
Kinyerezi”, alisisitiza Mgalu.
Pia alikagua ghala za kuhifadhia vifaa mbalimbali vinavyotumika katika
ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme lililopo Kibaha mkoani Pwani na
kushuhudia uwepo wa vifaa vya kutosha kukamilisha ujenzi wa njia hiyo.
Aidha aliwataka wasimamizi wa mradi huo kuwalipa vizuri wafanyakazi
/vibarua wanaofanya kazi katika mradi huo ili na wao wafurahie na
kunufaika kuwepo kwa mradi huo, vilevile aliwataka vibarua hao kufanya
kazi kwa bidii, kuwa walinzi wa vifaa hivyo na miundombinu na kuweka
mbele maslahi ya taifa.
Aidha alilipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi nzuri
ya kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme mkubwa katika reli ya kisasa, na kuwataka kuongeza kasi zaidi ya
ujenzi huo ili ikiwezekana ujenzi huo ukamilike kabla ya muda waliopewa.
Kwa upande msimamizi wa mradi huo kutoka Tanesco, Mhandisi
Deogratius Msaki alisema kuwa kazi hiyo inaendelea vizuri licha ya
changamoto ya kigiografia ya ardhi katika baadhi ya maeneo na hali ya
hewa ya mvua.
Aliweka wazi kuwa mpaka sasa tayari wamesimamisha nguzo zaidi 120
kati ya 456 zitakazotumika kutoka Dar es salaam hadi Morogoro, pia kazi
ya kuweka vikombe na kuanza kuvuta nyaya imekwisha anza katika
maeneo ambayo tayari usimikwaji wa nguzo umekamilika huku kazi hiyo
ikiendelea, matarajio yao ni kuukabidhi mradi huo Tar 28 Februari 2020.