Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika ,akizungumza wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma leo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma ,Gilles Muroto,akifatilia Mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma leo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo akitoa taarifa ya utekelezaji ya TAKUKURU Wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma leo
Baadhi ya viongozi wa TAKUKURU wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi hao uliofanyika jijini Dodoma leo.
………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Taasisi za kuzuia na kupambana na Rushwa hapa nchini TAKUKURU, imetakiwa kujipanga kwa ajili ya uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 2020, ili wapatikane viongozi ambao hawatokani na rushwa.
Wito huo umetolewa leo ijini Dodoma na Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora, Kapteni Msitaafu George Mkuchika, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa TAKUKURU, wenye lengo la kutathmini na kuweka malengo mapya.
Waziri Mkuchika amesema pamoja na kuwa wamefanikiwa katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa,huo uchukuliwe kama kipima joto kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao ambao kuna rushwa nyingi.
Waziri Mkuchika amesema uchaguzi huo ni muhimu sana kwa sababu ndio unachagua viongozi wa ngazi ya juu akiwemo Rais, Wabunge na viongozi wengine hivyo ukichagua wala rushwa itakuwa vigumu kuliongoza taifa hususani kwenye usimamiaji wa haki.
“Rushwa katika uchaguzi ni zaidi ya udanganyifu wa hesabu za kura, ambayo ikitendekea inasababisha kukosa viongozi waadilifu,wazalendo na wenye uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa,”
“kwahiyo ni lazima tujipange katika uchaguzi huo kuhakikisha vitendo vya Rushwa havipati nafasi kabisa kabla, wakati na Baada ya Uchaguzi huo” amesema Waziri Mkuchika.
Mbali na hilo Mkuchika amewataka Takukuru kuweka mkazo katika suala la rushwa ya ngono ambalo limekuwa kero na kusababisha watu wengi kukosa haki zao, licha ya kila kukicha katika vyombo vya habari kutiliwa mkazo
“Nawaomba TAKUKURU simamieni rushwa ya ngono vyuoni na kwingineko,hivi karibuni Makamu Mkuu wa Chuo kikuu UDOM alikiri rushwa ipo vyuoni,hivyo fuatilieni na kuwataka wanafunzi wa kike nao kutoa taarifa pale wanapokutana na rushwa hizo,”amesema Mkuchika.
Amesema imefahamika watuhumiwa ambao wanalawiti watoto wakikamatwa wazazi wanakaa meza moja kujadili suala hilo na kulimaliza bila hatua yoyote kuchukuliwa jambo ambalo halikubaliki.
“Ikibainika mzazi anafanya kitendo hiko yeye na mtuhumiwa wote watachukuliwa hatua kali,”amesema Mkuchika.
Amesema wanawake wapo wengi iweje mwanaume aende kubaka watoto au kulawiti na kuwasababisha magonjwa ya kuambukiza vijana wadogo ambao ni taifa la kesho.
Akizungumzia vyama vya ushirika,Mhe. Mkuchika amesema, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na TAKUKURU lakini bado yapo malalamiko mengi ya wakulima kutolipwa kwa wakati, kudaiwa rushwa ili waweze kulipwa, vyama kupokea fedha na kutowalipa kabisa baadhi ya wakulima, ukosefu wa uadilifu kwa viongozi na watumishi wa Vyama vya Ushirika ikiwa ni pamoja na kujilimbikizia mali.
“Ninawataka TAKUKURU mfuatilie na kuchukua hatua stahiki ili Vyama vya Ushirika visiwe ni kichaka cha wala rushwa,” amesisitiza Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Generali John Mbungo amesema katika tathmini ya utendaji wao mwaka huu wamefanikiwa kwa asilimia 88.1 kitu ambacho ni kiwango cha juu kuwahi kufikia.
Amesema kutokana na agizo la Rais Dk John Magufuli la kukusanya fedha za wakulima wa ufuta zilizoibiwa na vyama vya ushirika wamefanikiwa kukusanya sh zaidi ya million 900 ambazo zitakabidhiwa kwa wakulima.
Amesema awali Rais Magufuli amesema wakulima hao waliibiwa sh million 423 na vyama 10 vya ushirika,lakini katika uchunguzi wa Takukuru wamebaini sh billion 1.43 ambazo zimeibiwa na vyama 31 vya ushirika.
“Tumebaini ni vyama 31 vya ushirika na fedha zilizoibiwa ni zaidi y sh billion moja na hadi sasa milioni 900 tayari zimereshwa na zilizosalia zitarejeshwa zote kwa sababu tarehe ya mwisho ni leo ,”alisema Mbungo.
Mbali na hilo amesema jumla ya miradi 1,106 katika sekta ya maji,elimu,Afya na ujenzi ambayo inathamani y ash Trion 1.5,katika ufuatiliaji wao kiasi cha sh billion 43.3 kimebainika kufanyiwa ubadhilifu na hatua stahiki dhidi ya wahusika zinaendelea kuchukuliwa.
Amesema sh billion 23.7 zimeokolewa kutokana na oparesheni mbalimbali za uchunguzi na uzuiaji rushwa na kuongeza kuwa mali zenye thamani y ash billion 10.1 zilizopatikana kwa njia ya rushwa zimetaifishwa na mali za washtakiwa zenye thamani y ash billion 25.27 na Dola za Marekani million 5.67ziliwekewa zuio kwa lengo la ukamilishaji wa taratibu za kisheria kwa ajili ya utaifishaji wake.
Mbali na hilo alisema katika utekelezaji wake kesi 497 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini,zikiwemo rushwa kubwa nne zilizofunguliwa katika mahakama ya mafisadi nchini,ambapo kati ya hizo wameshinda kesi 206 ambapo ni sawa na asilimia 60.4 jambo ambalo ni mafanikio makubwa.