Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akihutubia kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge hivi karibuni.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge wakiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani hivi karibuni.
………………………………………………
NA TIGANYA VINCENT
MADIWANI na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge wametakiwa kuachana na mpango waliokusudia wa kutenga Kituo cha ukusanyaji wa asali bali wafikirie wazo la ujenzi wa Kiwanda cha kusindika asali ili kuongeza thamani ya asali hiyo
Ushauri huo umetolewa juzi wilayani Sikonge na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani.
Alisema utaratibu wa ujenzi wa Kiwanda utawasaidia wafugaji wa nyuki kupata faida kubwa na kuwa na bidhaa ambazo zinajulukiana asili yake zinazalishwa na Kiwanda cha Sikonge(Made in Sikonge)
Mwanri alisema kitendo cha kuruhusu Sikonge kugeuka kuwa sehemu ya kukusanya asali ambayo haijasindikwa utasababisha watu kutoka nje kuingia katika eneo la kukusanya asali yote na kuwaacha wafugaji wakiwa na faida kidogo huko ikienda kunufaisha maeneo mengine.
“ Naona Sikonge hatuelewani mimi nazungumzia uanzishaji wa Kiwanda cha kusindika asali na kuiweka kwenye vifungashio kama vile Chupa ambazo zina nembo ya Sikonge, nyie mnafikiria kuwa na ‘collection centre’ ambapo asali itauzwa kabla ya kuongezewa thamani na kwenda kunufaisha watu wa sehemu nyingine na kuwacha watu wakiwa maskini “ alisema.