Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Sophia Jongo akizungumza leo Desemba 5,2019 kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia,ambapo kilele chake kitafanyika Desemba 10 mwaka huu. Picha zote na Marco Maduhu – Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Shirika la Agape mkoani Shinyanga John Myola akizungumza kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi wa Shirika la Equality For Growth (EFG) kutoka Jijini dar es salaam Jane Majigita, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Shinyanga Grace Salia akizungumza kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
Afisa Maendeleo ya Jamii manispaa ya Shinyanga Anjel Mwaipopo akizungumza kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Wanafunzi pamoja na Askari Polisi wakiwa kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwenye viwanja vya Zimamoto Shinyanga Mjini.
Wanafunzi pamoja na askari Polisi wakiwa kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwenye viwanja vya Zimamoto Shinyanga Mjini.
Wanafunzi wakiwa kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Mwenge wakitoa burudani.
Burudani ikiendelea kutolewa kwenye maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kucheza na nyoka.
Kiongozi wa kikundi cha ngoma, Mahona Mtoba, akitoa burudani Meza kuu.
Awali wanafunzi wakiandamana kutoka Bwalo la Polisi hadi kwenye viwanja vya Zimamoto kwa ajili ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Maandamano yakiendelea.
Wanafunzi wakionyesha mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Mgeni Rasmi akipokea maandamano pamoja na meza kuu.
Mgeni rasmi kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Sophia Jongo akipiga picha ya pamoja na wafanyakazi kutoka Shirika la Agape, pamoja na mkurugenzi wa Shirika la EFG, Jane Majigita (wa kwanza mkono wa kushoto aliyekaa kwenye kiti).
***
Shirika lisilo la kiserikali Agape Aids Cotrol Program la mkoani Shinyanga, limefanya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kupinga vitendo vya ubakaji, ulawiti, mimba na ndoa za utotoni, pamoja na kutoa lugha chafu za matusi kwa wafanyabiashara wanawake sokoni.
Maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni Desemba 10 mwaka huu, yamefanyika kwenye viwanja vya Zimamoto Shinyanga mjini leo Desemba 5,2019 ambapo mgeni rasmi alikuwa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Sophia Jongo.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo ,Kamanda Jongo, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuacha tabia ya kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wadogo, ikiwemo ubakaji, ulawiti, vipigo, kuwapa mimba pamoja na kuwaozesha ndoa za utotoni.
Amesema mkoa wa Shinyanga unashika nafasi ya tano kitaifa dhidi ya matukio ya ubakaji, ikiwamo wanafunzi kupewa ujauzito pamoja na kuozeshwa ndoa za utotoni, jambo ambalo linauchafua mkoa, na hivyo kuwataka wananchi waachane na matukio hayo ili watoto wapate kusoma kwa bidii na kuweza kutimiza ndoto zao.
“Nayapongeza sana mashirika haya ambayo siyo ya kiserikali likiwamo la Eguality For Growth (EFG) pamoja na Shirika la Agape, kwa kazi nzuri sana ambayo wanayoifanya mkoani hapa kwa kupambana kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto,”amesema Jongo.
“Pia naomba waendelee na mapambano haya ya kutokomeza ukatili huu wa kijinsia, kwa kutoa elimu kwa wananchi pamoja na wanafunzi dhidi ya madhara haya ya kufanya ukatili, ambapo mkoa wetu unaongoza kwa matukio ya ubakaji watoto na tunashika nafasi ya tano kitaifa,”ameongeza.
Naye mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola, amesema Shirika hilo limekuwa likijihusisha na miradi mbalimbali ya kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo miradi ya kupinga mimba na ndoa za utotoni, pamoja na ukatili dhidi ya wanawake sokoni.
Pia amelipogeza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana vyema na Shirika hilo la Agape dhidi ya mapambano ya matukio ya ukatili, ambapo wao wanapokuwa wakitoa taarifa za matukio hayo, polisi hufika mara moja kwenye eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Equality For Growth kutoka Jijini Dar es salaam Jane Majigita, ametoa wito kwa wananchi pamoja na watoto, wawe wanatoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia, ili yafanyiwe kazi na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria, hali ambayo itapunguza matukio hayo.
Aidha kauli mbiu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mwaka huu inasema “Kizazi Chenye Usawa, Simama Dhidi ya Ubakaji”.