Mkuu wa Kitengo cha Usalama,Majanga ya Moto na Uchunguzi Naibu Kamishna Fikiri Salla, akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji(hawapo pichani), wakati akifungua mafunzo ya namna mifumo ya kinga na tahadhari dhidi ya moto inavyofanya kazi kwenye mabasi aina ya Yutong. Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango, Jijini Dodoma yakiendeshwa na Wakufunzi kutoka Kampuni ya kutengeneza mabasi aina ya Yutong.Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Mkufunzi kutoka Kampuni ya Mabasi ya Yutong Lang Chang Ling akitoa ufafanuzi jinsi mifumo ya kinga na tahadhari dhidi ya moto inavyofanya kazi kwenye mabasihayo kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma ,leo ambapo mafunzo hayo ya siku mbili yameanza.Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
*********************************
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya kutengeneza Mabasi aina ya Yutong imetoa mafunzo kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji nchini, namna mifumo ya kinga na tahadhari dhidi ya moto inavyofanya kazi katika mabasi hayo yanayofanya safari zake mikoani na nje ya nchi ili kuweza kujikinga pindi yanapopata hitilafu na kuwaka moto lengo ikiwa ni kupunguza ajali za moto.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango, Jijini Dodoma yamefunguliwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Usalama,Majanga ya Moto na Uchunguzi,Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,Fikiri Salla huku washiriki hao wakifundishwa nadharia na vitendo katika kudhibiti majanga ya moto na
ikiwa pamoja na kuangalia mifumo ya magari hayo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Naibu Kamishna Fikiri alisema sasa ni wakati wa sayansi na teknolojia na jeshi halina budi kuanza kujifunza njia mbalimbali za udhibiti wa majanga kwa kutumia teknolojia huku akiishukuru kampuni ya Yutong kwa mafunzo hayo.
“Tunapitia kipindi cha mabadiliko ya sayansi na teknolojia naamini mafunzo haya yatawawezesha askari wetu kujifunza njia hizo za kisasa sambamba na kuelewa mfumo mzima wa mabasi hayo ambayo yamekua mengi hivi sasa hapa nchini na yakitumika katika usafiri wa kwenda mikoa mbalimbali” alisema Naibu Kamishna Fikiri
Aidha mafunzo hayo yanaendeshwa na Wakufunzi kutoka Kampuni ya
kutengeneza mabasi aina ya Yutong wakiongozwa na Meneja Huduma wa Kampuni hiyo, Lang Chang Ling,Mtaalamu wa Usalama kwenye gari,Ma Jiong na Mhandisi wa Huduma, Zhao Le Hui
Wakiongea kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo ya siku mbili walisema wanaamini baada ya mafunzo kumalizika watakua wamepata elimu ambayo itawaongezea kitu katika shughuli zao za kila siku zinazohusiana na majanga ya moto na uokoaji.