Home Biashara WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUONYESHA TIN ZAO

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUONYESHA TIN ZAO

0

Afisa wa TRA Bi. Oliver Njunwa akitoa elimu kwa wafanyabiashar wa Kivule, Ilala jijini Dar es salaam.

Meneja wa Hudumakwa Mlipakodi Bi. Honesta Ndunguru akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya wananchi wa Kivule wakati wa kampeni ya elimu na huduma kwa mlipakodi.

Afisa wa Kodi Alex Mwambenja akitoa elimu kwa wafanyabiashara wa Kivule, Ilala Dare es salaam.

****************************************

Wafanyabiashara wametakiwa kuweka cheti cha namba ya utambulisho wa Mlipakodi (TIN) mahali ambapo kinaonekana vizuri katika katika maeneo yao ya biashara.

 

Wito huo umetolewa na Meneja wa Huduma wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi Honesta Ndunguru baada ya kubaini kwamba baadhi ya wafanyabiashara hawaweki cheti cha TIN katika sehemu zao za biashara pamoja na kutakiwa kufanya hivyo wakati wote wanapofanyabiashara.

 

Bi. Ndunguru alikuwa anaongea na wafanyabiashara wa Kivule Wilaya ya Ilala katika mkoa wa Dar es salaam wakati wa kampeni ya huduma na Elimu ya kodi inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam kuhamasisha wananchi kulipa kodi, kusajili na kulipa kodi ya majengo kusajili biashara na kupatiwa namba ya utambuliso wa mlipakodi pamoja na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha zaidi huduma zinazotolewa na TRA.

 

Pia amewasihi wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutumia fursa hiyo ambayo TRA inakuwa karibu zaidi kuwapa elimu na kutatua changamoto zinazowakabili kwa kutembelea vituo ambavyo vimeainishwa pamoja na kutoa maelezo ambayo yatawasaidia TRA kutatua changamoto mbalimbali.

 

“Tunawaomba wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wajitokeze kwa wingi na wasisite kuuliza maswali, kutoa maoni ya kuboresha huduma ili mazingira ya kulipa kodi yawe rahisi na rafiki na hivyo kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla”, amesema Bi Ndunguru .

 

Kwa upande wao wananchi katika maeneo ya Kivule wamepongeza zoezi la huduma na elimu wakisema kwamba kwao ni fursa nzuri ya kupata huduma ambazo ingewagharimu kuzifuata katika vituo vya TRA. Wameiomba TRA kufanya kampeni hiyo mara kwa mara ili iwe kama njia ya kuwakumbusha kulipa kodi hususan kodi ya majengo.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao wa Kivule wamesema kwamba kitendo cha kutembelewa na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika sehemu zao za biashara na makazi kutoa elimu ni cha kupongezwa kwani kinawaondolea hofu na kujenga urafiki kati yao na TRA.

 

“Hatuna sababu ya kuwakimbia TRA au kufunga biashara kwani tumepata fursa ya kuelimishwa na kupata ufafanuzi wa mambo ambayo tulikuwa hatufahamu”, anasema Esthar Charles mfanyabiashara katika eneo la Kivule.

 

Wakiwa katika eneo la Kivule maofisa wa TRA katika siku mbili za kampeni ya huduma na elimu ya kodi wamefanikiwa kutembelea zaidi ya wafanyabiashara 100 na majengo 100 huku wananchi wengi wakijitokeza kupata ankara zao za majengo na kusajili majengo yao na hatimayekulipa kodi ya majengo.

 

Kampeni ya huduma na elimu kwa mlipakodi ni zoezi ambalo linaendeshwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kutembelea maeneo ya wafanyabiashara na
wananchi wenye majengo mlango kwa mlango kuwapa elimu na kusikiliza kero,
changamoto na maoni.

 

 

Tayari zoezi hili limefanyika wa mafanikio katika mikoa ya Morogoro na Pwani na sasa linaendelea katika mkoa wa Dar es salaam hadi tarehe 14 Novemba 2019.