Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Uchukuzi, Hassan Hemed (wa
pili kulia) jana akimkabidhi Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire (wapili kushoto) moja ya
vikombe 14 vya ushindi wa mashindano ya Mei Mosi yaliyofanyika Mei 2019
mkoani Mbeya. Katikati ni Katibu Mkuu wa klabu hiyo Mbura Tenga.
Viongozi mbalimbali wa Klabu ya Uchukuzi wakishughudia
makabidhiano ya vikombe 14 vya ushindi wa mashindano ya Mei Mosi
yaliyofanywa jana na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Hemed
(mwenye shati la Kitenge) akimkabidhi Kaimu Katibu Mkuu wa Sekta ya
Uchukuzi, Gabriel Migire.
***********************************
Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), imeipa tano timu yake ya Uchukuzi baada ya kufanya vyema kwenye mashindano ya Mei Mosi yaliyofanyika mapema mwezi Mei, 2019 mkoani Mbeya.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migire, kwa niaba ya Mlezi wa timu hiyo, Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, wakati akipokea vikombe tisa (9) vya ushindi wa michezo mbalimbali, ambapo miongoni mwa hivyo vinne vimetolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema timu hii imeweza kufanya vyema na kuonesha dhahiri pamoja na maandalizi ya muda mfupi.
“Hongereni ushindi wenu unatupa moyo kama uongozi wa Wizara, hata kwa kiwango kidogo Wizara imefanya matokeo yamekuwa makubwa sana, tunashukuru mmetubeba na imeonekana kuna kitu mnafanya kitu hili sio jambo dogo ni kubwa sana hadi Mhe Rais katambua kuna kazi imefanyika hadi kutoa vikombe hivyo.” Amesema.
Amesema wizara itashughulikia changamoto zote zinazoikabili klabu hiyo, ili kuboresha shughuli zote za michezo, ili kufanikisha ushindi zaidi.
Hatahivyo, amesema taasisi zote zinazounda timu hiyo zinatakiwa kutenga bajeti ya michezo katika bajeti zao za mwaka ili ziweze kutoa wachezaji watakaowakilisha sekta hiyo.
Awali Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mbura Tenga amesema klabu hiyo iliyokuwa na wachezaji 99 kutoka Wizarani na taasisi zilizopo chini ya sekta hiyo, walishiriki kwenye michezo yote 14 ikiwemo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, karata, bao, draft, riadha na baiskeli (wanawake na wanaume).
Tenga amesema wameweza kutwaa vikombe vinne (4) vya ushindi wa kwanza, huku vikombe viwili (2) vimetwaliwa katika ushindi wa pili na vitatu (3) vya ushindi wa tatu.
“Kutokana na vikombe hivyo tisa timu yetu ya Uchukuzi iliweza kutawazwa kuwa Bingwa wa Jumla wa mashindano hayo, kwa kuwa hakukuwa na timu nyingine iliyoweza kutwaa vikombe vingi kama vyetu.” Amesema Tenga.
Hatahivyo, Tenga amesema pamoja na timu kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa zikiwemo jezi, mipira na sare za ujumla, bado ameahidi wataendelea kufanya vyema kwenye michezo yote pamoja na mabonanza watakayoalikwa.
Amesema hivi karibuni klabu itatangaza ratiba ya kuanza kwa mazoezi ya kujiandaa na michezo ya Mei Mosi na mabonanza mengine ikiwemo kuzialika taasisi zinazoshughulikia Uchukuzi za Zanzibar ili kudumisha Muungano.
Akizungumzia ushiriki wa timu hiyo katika michezo mingine, kuwa imeweza kushiriki katika Bonanza la Kuadhimisha Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Zanzibar (ZAA) lililofanyika Agosti, 2019 Visiwani Pemba, kwa kushirikisha watumishi 45 kutoka taasisi mbalimbali.
Halikadhalika, ameiomba Wizara kuridhia tarehe 30 Juni 2020 kufanyika kwa Bonanza kubwa la Sekta hiyo litakaofanyika mkoani Dodoma.