Home Siasa MWENYEKITI UVCCM MTWARA ANG’OLEWA UONGOZI KWA KUDANGANYA UMRI

MWENYEKITI UVCCM MTWARA ANG’OLEWA UONGOZI KWA KUDANGANYA UMRI

0

Na.Alex Sonna,Dodoma

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Mtwara, Aziz Mrope amevuliwa nafasi hiyo pamoja na kufutiwa uanachama wa umoja huo baada ya kubainika kuwa amedanganya umri.

Uamuzi wa kumvua madaraka  umetolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James baada ya mkutano wa umoja huo kupitisha maamuzi hayo  jijini Dodoma.

Bw.James akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mkutano huo amesema kuwa uamuzi umefikiwa na  mkutano mkuu kujiridhisha kuwa Mrope alifanya udanganyifu kwenye umri.

” Kwa umoja wetu ambayo tumejadili katika Mkutano mkuu tumeridhia kwa pamoja kumfuta uanachama Bw.Mrope kwa udanganyifu na tumemuondoa katika nafasi yake ya uongozi aliyokuwa nayo, hivyo niuagize Mkoa wa Mtwara kuanza mara moja mchakato wa kujaza nafasi hiyo ambayo iko wazi,” Amesema Kheri.

Aidha alizungumzia ziara ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Bashiru Ally aliyoifanya visiwani Zanzibar  amesema kuwa ilikuwa ziara ya kuimarisha uhai wa Chama na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 Visiwani Zanzibar.

” Tumemsikia mzee mmoja anaitwa Maalim Seif anahoji uhalali wa Dk Bashiru, tumpe taarifa tu kuwa Katibu Mkuu ataendelea kufanya ziara hizo ambazo zina tija kwa Chama chetu na Serikali lakini pia akimaliza yeye na sisi vijana pamoja na Jumuiya za Wazazi na Wanawake tutafanya ziara zetu,” Amesema Kheri James.

Hata hivyo Bw.James amewapongeza viongozi wa Mikoa wa UVCCM na wanachama wao kwa kuhakikisha kuwa CCM inashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Amewataka kuendelea kutangaza kazi kubwa inayofanywa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe Rais Dk John Magufuli ili kumtengenezea njia rahisi ya kupata kura nyingi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

” Sisi kama vijana moja ya majukumu yetu ni kuwa  mabalozi wa kazi nzuri inayofanywa na serikali yetu chini ya Mzalendo Dkt Magufuli, twendeni kazini tukatangaze yote yaliyofanywa na Serikali yetu ambayo ni ya Chama chetu.