Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (Mb.), ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuchunguza utaratibu uliotumika kuendesha Mashindano ya kimataifa ya mbio ndefu ya Kigamboni (Kigamboni International Marathon) yaliyofanyika leo asubuhi
jijini Dar es Salaam kubaini uvunjifu wowote wa taratibu na dhamira ya michezo.
Dk. Mwakyembe ambaye yuko Mwanza ambako amezindua mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni binafsi (SHIMMUTA), ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa washiriki wa mbio hizo ndefu kutoka ndani na nje ya Dar es Salaam.
Waziri amesema kuibuka kwa mashindano mengi ya mbio ndefu nchini ni faraja kubwa kwa Taifa, lakini mashindano hayo yasiwe kichochoro kipya cha utapeli nchini cha kuwavunja moyo Watanzania wenye nia njema ya michezo na ameagiza hatua kali zichukuliwe kudhibiti uvunjifu wowote wa taratibu.
Taarifa zilizomfikia Waziri ni kuwa mbio hizo za Kigamboni ziliendeshwa bila ushiriki wa Shirikisho la Riadha nchini na zawadi zilizotolewa kwa washindi wa kwanza mpaka wa tatu zilikuwa za kutweza ( sh.150,000; 80,000; na 60,000) kwa mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu kwa mbio za kilomita 22 na kila mshiriki alilipia sh. 25,000/= kupata namba ya ushiriki.