Na Alex Sonna,Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania na ilianza kufanya kazi Septemba 2006.
Inadhibiti huduma za nishati (Umeme, Petroli na Gesi asilia) na Maji na Usafi wa Mazingira na udhibiti wa sekta hizi kwa pamoja unapunguza gharama za udhibiti na kuwezesha mapato ya tozo ya sekta ya nishati kugharamia sehemu ya gharama za udhibiti wa sekta ya maji.
Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini iliandaa Mfumo wa Uagizaji wa Pamoja (BPS) wa mafuta nchini.
Katika utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM), Aprili 2014,ulibaini kuokolewa kwa Sh.Bilioni 121.6 kwa 2012 na 2013.
Akizungumzia mafanikio na changamoto ya sekta ndogo ya mafuta, katika warsha ya waandishi wa habari hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany, anasema kumekuwepo na mafanikio mbalimbali kupitia mfumo huo ikiwemo kuokolewa kwa kiasi hicho cha fedha.
“Pia kupungua kwa gharama za usafirishaji na
Premium (TZS 81.9 bilioni katika kipindi cha miaka miwili), kupungua kwa gharama za demurrage kwa TZS 25.7 bilioni, kupungua kwa “ocean losses” kwa TZS 14 bilioni baada ya kubadilisha taratibu za uagizaji mafuta kutoka “Cost, Insurance and Freight” na kuwa
“Delivery at Port”,”anasema.
FAIDA YA BPS
Akizungumzia faida nyingine za uagizaji wa mafuta kwa pamoja kuwa ni kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi za ujazo wa mafuta yanayoingizwa nchini.
“Kurahisisha ukokotoaji wa bei za mafuta kwa mtindo ulio wazi zaidi,kurahisisha udhibiti wa ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini kwa mfumo huu, Mfumo wa BPS utaendelea kuleta manufaa makubwa kwa nchi, wadau na wananchi kwa ujumla,”anasema.
Kaimu Mkurugenzi huyo anasema ni muhimu ukaendelezwa mfumo huo na taratibu zake zikazingatiwa na wadau wote.
UBORA WA MAFUTA
Mchany anasema uchakachuaji wa mafuta ni changamoto kubwa hapa nchini.
“EWURA imepambana na tatizo hili ambapo uchakachuaji umepungua kutoka asilimia 78 mwaka 2007 hadi asilimia 4 sasa,”anasema
Aidha, anasema Septemba 2010, EWURA ilianzisha Program ya kuweka vinasaba kwenye mafuta yanayotumika nchini ili kudhibiti uchakachuaji na ukwepaji kodi (fuel dumping) na kuweka mazingira ya ushindani wa haki.
“Utafiti wa UDSM kuhusu matumizi ya vinasaba kwa mwaka 2010 – 2013 ulibaini ongezeko la mapato ya Serikali (kodi) kwa TZS 468.50 bilion, Manufaa haya yanaendelea kupatikana,”anasema
UBORA WA MIUNDOMBINU YA MAFUTA
Anasema EWURA inadhibiti ubora wa miundombinu ya mafuta kwa ili kulinda afya, usalama na mazingira (HSE).
“Kutokana na udhibiti wa EWURA, maghala na vituo vya mafuta vimeendelea kuwa bora zaidi, pia EWURA imeandaa masharti nafuu ili kuvutia wawekezaji kwenye maeneo ya vijijini.”anasema
TAHADHARI MUHIMU MATUMIZI MAFUTA
Anasema kuna tahadhari mbalimbali za matumizi ya mafuta zinapaswa kuzingatiwa ikiwamo magari ya kubebea mafuta kutoegeshwa au kulazwa pasipo husika na badala yake yawekwe sehemu maalumu zilizotengwa.
Mchany anataja tahadhari nyingine ni kuwa shughuli zote zinazohusu mafuta ya petroli ni lazima zifanyike kwa umakini na uangalifu mkubwa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Anaeleza kuwa ni muhimu kuzingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Viwango vya ubora na masharti ya leseni wakati wote.
“Tahadhari kubwa zinatakiwa kuchukuliwa katika shughuli za utunzaji, usafirishaji na utumiaji/uuzaji wa bidhaa za petroli, pamoja na kuhakikisha kuwa maeneo yanayotumika yameruhusiwa kwa matumizi ya shughuli za
mafuta,”anasema
Aidha anasema “Miundombinu kama vile magari ya kubebea bidhaa za petroli, vituo vya mafuta, maghala makubwa ya kuhifadhia, vijengwe/au kuundwa kwa ubora unaotakiwa na kuendeshwa kwa kufuata kanuni za kiusalama, kiafya na kimazingira.”
Mchany anafafanua kuwa miundombinu yote inatakiwa kila wakati iwe na vifaa vya Kuzimia moto na viwe vinafanya kazi.
Anasema inabidi wafanyakazi wafundishwe jinsi ya kutumia vifaa hivyo endapo moto unatokea ili kukabiliana nao.
Pia, anasema madhara makubwa yanaweza kusababishwa na mlipuko wa gari linalobeba mafuta.
“Wananchi wasisogelee gari la mafuta hasa linapopata ajali, magari ya kubebea mafuta yasiegeshwe au kulazwa pasipohusika- yaegeshwe na kulazwa sehemu maalumu
zilizotengwa,”anasema.
Anasisitiza kwa wakati wote vifaa vya kuhifadhia, kubebea na kusafirishia mafuta vikaguliwe na kuwekwa katika viwango bora.
Mbali na hilo anasema lazima kuweka alama za tahadhari katika maeneo yanayohusika na shughuli za mafuta mfano usivute sigara, zima injini, zima simu, vaa vifaa vya usalama uingiapo mahali hapa.
UTOAJI LESENI
Anafafanua kuwa Ewura imetoa leseni 1,561 za biashara ya mafuta zikiwemo leseni za Biashara ya Mafuta ya Jumla 66, Biashara ya Mafuta ya Rejareja 1,397 na leseni 19 kwa gesi ya kupikia na vilainishi vya mitambo ni 56.
VITUO TEMBEZI VYA MAFUTA
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo ya Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo anasema Ewura imeibuka na mkakati mpya wa kuanzisha vituo vya mafuta vinavyotembea (mobile fuel system) kwa kutumia magari maalumu yaliyotengenezwa kwa kazi hiyo.
Anasema mpango huo unalenga kurahisisha upatikanaji wa mafuta katika maeneo mbalimbali nchini yakiwamo ya vijijini.
“Nishati ya mafuta inatakiwa kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika na kwa kuwa kujenga visima vikubwa ni gharama, njia hiyo ni bora na itakuwa ni rahisi kuwafikia wateja walio wengi,” anasema Kaguo.
Anasema katika maeneo mengi nchini wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakisafirisha na kuuza mafuta kwa njia ambazo si sahihi na zinazohatarisha usalama wa vyombo vya watumiaji na maisha yao wenyewe.
Anafafanua kuwa watu wanatakiwa kufahamu kuwa kusafirisha kuuza mafuta kwa njia zisizo rasmi kwa kutumia madumu ni kosa kisheria na pia ni hatari kubwa inayoweza kusababisha majanga kama milipiko ya moto.
‘’Kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri kama pikipiki, tumeamua kupunguza gharama za kuanzisha vituo vya uuzaji mafuta ili viweze kujengwa katika maeneo mbalimbali hasa vijijini ili kuepuka uuzaji mafuta katika vidumu,” anasema.