Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama(kushoto) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Haruna Kasele(katikati) jana kabla ajafungua mafunzo ya siku mbili ya Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na wajumbe wa Serikali za Vijiji waliochaguliwa hivi karibuni wilayani humo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Haruna Kasele akiwasisitiza jana Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji juu ya kushirikiana na Madiwani katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
………………..
NA TIGANYA VINCENT
SERIKALI imewaagiza viongozi wa Serikali za Mitaa walioapishwa kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ajili ya kupata fedha za kuwaletea maendeleo wananchi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Wajumbe wa Wilaya ya Kaliua waliochaguliwa hivi karibuni na kuapishwa.
Alisema kuwa kazi kubwa iliyopo mbele yao ni kuhakikisha wanakusanya ushuru, kodi ,maduhuli na mapato mengine ya Serikali katika maeneo yao.
Mwanri aliongeza kuwa jukumu lao jingine ni kuratibu shughuli na miradi mbalimbali katika maeneo yao ya Vitongoji na Vijiji kwa ajili ya kuhakikisha matumaini na matarajio ya wananchi yanatimizwa.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Haruna Kasele aliwataka viongozi wa vitongoji na vijiji waliochaguliwa hivi karibuni kutumia Sheria ndogo ndogo za Vijiji katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali yaliyo ndani ya uwezo wao.
Aidha aliwataka kushirikiana na Madiwani katika kuhakikisha wanahamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, Zahanati na utengezaji wa barababara za Vijiji.