*************************************
NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA
Mkoa wa Pwani, umefanya mnada wa kwanza wa korosho kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kufanikiwa kuuza korosho yote iliyokuwa katika maghala makuu, kilo 156,257 kwa daraja la kwanza na la pili.
Aidha baadhi ya waendesha maghala wamekewa kuacha kupokea cha juu kwa viongozi wachache wa AMCOS ambao sio waaminifu ,wakitaka wapokee korosho zisizo na viwango ama kupewa stakabadhi za ghala wakati hakuna korosho zilizopelekwa kwenye maghala yao.
Akizindua mnada huo huko Mkuranga ,mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo alisema, daraja la kwanza limeuzwa kwa bei ya sh.2,571 ambapo korosho hizo zimenunuliwa na kampuni ya Alpha Choice.
Alieleza, daraja la pili limenunuliwa kwa bei sh.2,300 na korosho hizo zimenunuliwa na kampuni ya CDJKL.
Hata hivyo, Ndikilo aliwataka wakulima kukausha korosho zao ili ziwe kavu na zenye ubora na wakati wa msimu wa kilimo kupalilia na kufufua mikorosho ya zamani ili kujiongezea kipato.
Ndikilo hakusita kubainisha kwamba ,licha ya juhudi zote hizo mapokezi ya hali ya korosho kwenyw maghala hairidhishi hivyo ukusanyaji uongezeke ili kufanya mnada wa pili na mingine yenye mafanikio kwa wakulima.
“Lindi imeshafika mnada wa saba,sisi ndio tumeanza ,tusifanye mchezo katika masuala ya uchumi ama lenye manufaa kwetu kama hili”alisisitiza .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo alisema wilaya hiyo ina korosho kilo 107,592 na ubora ni STD na UG na uhakiki unaendelea.
Nae mrajisi wa mkoa wa Pwani, Angela Nalimi aliweka bayana kuwa, mkoa unapendekeza korosho zenye ubora stahili zitaendelea kupokelewa kwenye maghala makuu.
Alisema korosho nyingi pia bado zipo katika maghala ya AMCOS ambapo yatasimamiwa na kuratibiwa na chama kikuu (CORECU)
Angela alieleza ,halmashauri kupitia ofisi za ushirika zitasimamia malipo ya wakulima wote waliokusanya korosho kupitia AMCOS.