Albeto Mweta mkazi wa Kijiji cha Ighaka wilayani Ikungi mkoani Singida, akionesha mabaki ya nyumba yake inayodaiwa kubomolewa na Kampuni ya Udalali ya Majembe Auction Mart bila ya kufuata taratibu na kuiacha familia yake ya watu 15 kukosa mahali pa kuishi.
Hamisi Said Mdimu akizungumzia jinsi alivyopata eneo hilo linalo lalamikiwa.
Wananchi wakiwa nje ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi walipofika kuelezea jinsi wanavyofahamu historia ya eneo lenye mgogoro.
Mzee Seleman Mhandi akizungumzia historia ya eneo lenye mgogoro.
Albeto Mweta, akizungumzia jinsi alivyo bomolewa nyumba yake.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo amemuagiza mkuu wa polisi wa wilaya hiyo (OCD) kumkamata Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Majembe Auction Mart kwa kukiuka taratibu kwa kubomoa nyumba ya Albeto Mweta mkazi wa Kijiji cha Ighaka wilayani humo na kusababisha familiya yake kukosa mahali pa kuishi.
Katika hatua nyingine Mpogolo amemtaka mkazi mwingine wa kijiji hicho Hamisi Said kufika ofisini kwake mapema wiki hii akiwa na barua yenye uthibitisho wa kisheria uliompa mamlaka ya kusimamia kesi iliyompa ushindi na kuweza kuwapeleka maofisa wa Kampuni ya Udalali ya Majembe Auction Mart kwenda kubomoa nyumba hiyo kwa kumsainisha Mwalimu Halima Nguya ili asimamie zoeli hilo badala ya Afisa Mtendaji.
DC Mpogolo aliongeza kuwa maofisa wa kampuni hiyo walifika katika Wilaya ya Ikungi kuja kubomoa nyumba hiyo wakitokea wilaya nyingine ya Singida mjini pasipo kuripoti ofisi yoyote ya serikali au kwa OCD ili wajue na kujiridhisha kama zoezi hilo lilikuwa likifanyika kihalali au laa.
Mpogolo alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki wakati akisikiliza maelezo ya pande mbili kati ya Hamisi Said na Albeto Mweta ambao walikuwa na kesi ya kugombea shamba la ekari moja ambalo kila mtu akidai ni lake.
Hata hivyo kumekuwa na sintofahamu katika maamuzi ya mahakama kitengo cha ardhi mkoani hapa kumpa ushindi Hamisi Said wakati shamba hilo likidaiwa kuwa lilikuwa la mkwe wake Hassani Mwinyimvua ambaye kwa sasa ni marehemu.
Imeelezwa kuwa Hassani Mwinyimvua ana watoto wakubwa waliosoma na wananafasi kubwa za kazi serikalini alishindwaje kuwapa kazi ya kufuatilia shamba hilo badala yake ampe mkwe wake Hamisi Said.
Hamisi Said akizungumzia tukio hilo alisema eneo hilo lilikuwa na mkwe wake Hassan Mwinyimvua ambaye alimchagua kulifuatilia kama msimamizi na kuwa lilikuwa la urithi wa baba yake.
Mzee Seleman Mhandi ( 85) ambaye anajua historia ya maeneo hayo anasema hata wao hawajui jinsi Hassan Mwinyimvua alivvyopata eneo hilo lililopo ndani ya maeneo ya ukoo wa akina Mweta.
Albeto Mweta ambaye ni mlalamikaji wa kubomolewa nyumba yake anasema eneo hilo ni la urithi na alikabidhiwa na baba yake Colman Mweta tangu mwaka 1984.
Afisa wa Kampuni ya Udalali ya Majembe Aution Mart kutoka Dodoma aliyesimamia zoezi la kubomoa nyumba hiyo, Edwin Binamu alisema zoezi hilo walilifanya kisheria baada ya mahakama kutoa hukumu na kuwa walimsainisha Mwalimu Halima Nguya kwa kuwa alikuwa akikaimu nafasi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho ambaye kwa wakati huo alikuwa yupo likizo ya uzazi.