Home Mchanganyiko ZAIDI YA WAKULIMA 500,000 WAMEJENGEWA UWEZO CHINI YA MFUMO SHIRIKISHI WA UDHIBITI...

ZAIDI YA WAKULIMA 500,000 WAMEJENGEWA UWEZO CHINI YA MFUMO SHIRIKISHI WA UDHIBITI UBORA KWA AJILI YA SOKO LA NDANI NA LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

0

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua kongamano la kitaifa la kilimo-hai la siku mbili linalofanyika Jijini Dodoma tarehe 26 Novemba 2019. (Picha Zote Na Mathias canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua baadhi ya bidhaa za wajasiriamali wakati wa hafla ya uzinduzi wa kongamano la kitaifa la kilimo-hai la siku mbili linalofanyika Jijini Dodoma tarehe 26 Novemba 2019. 
Sehemu ya washiriki wa kongamano la kitaifa la kilimo-hai la siku mbili linalofanyika Jijini Dodoma tarehe 26 Novemba 2019 wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb).
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji  akisisitiza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kongamano la kitaifa la kilimo-hai la siku mbili linalofanyika Jijini Dodoma tarehe 26 Novemba 2019. 
 
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
 
Nchi
mbalimbali Duniani zinajadili na kuweka mikakati ya kuendeleza kilimo-hai. Mwaka
2010, Umoja wa Afrika kupitia Marais wake, ulipitisha Azimio la mpango na
mkakati wa kilimo-hai kuelekea ajenda yake ya miaka 50 ijayo (Agenda 2063), na
kuzitaka nchi zote kuchukua hatua kutekeleza azimio hilo.
 
Katika
kufikia azimio hili la Umoja wa Afrika, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na
wadau imefanikiwa kuwa na Sera ya Kilimo iliyohusisha kilimo-hai kwa upana wake
na uwekezaji kwenye viwanda vinavyo chakata mazao ya kilimo-hai.
 
Hii inaenda
sambamba na jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais John
Pombe Joseph Magufuli ya kutaka Tanzania ifikie uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025 kupitia sera ya viwanda. Ambapo kumeanzishwa dawati la kilimo-hai katika
idaya ya Maendeleo ya Mazao ili  kufikia
idadi ya wakulima  na wafugaji 149,000 waliothibitishwa
na kuingia katika fursa ya masoko ya bidhaa za kilimo-hai kimataifa,
wanaozalisha kwenye eneo la hekta takribani 278,000.
 
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo jana tarehe 26 Novemba 2019
wakati akifungua kongamano la kitaifa la kilimo-hai la siku mbili linalofanyika
Jijini Dodoma na kuongeza kuwa zaidi ya wakulima 500,000 wamejengewa uwezo
chini ya mfumo shirikishi wa udhibiti ubora (participatory guarantee system –
PGS) kwa ajili ya soko la ndani na la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Ameongeza
kuwa kilimo-hai Duniani katika mataifa mbalimbali kinakua kwa kasi kubwa.
Inakadiriwa kuwa soko la bidhaa na mazao ya kilimo-hai duniani ni wastani wa Euro
89 bilioni ambapo hiyo ni fursa kubwa kwa kwa Tanzania kwani ni nchi ya tatu
kati ya tano barani Afrika zinazoongoza kwa kuwa na eneo na idadi kubwa zaidi
zilizo thibitishwa katika mfumo huo wa kilimo-hai, ikiongozwa na Uganda na
Ethiopia na kufuatiwa na Kenya na Jamhuri ya Kidemokrsi ya Kongo (DRC).
 
Waziri
Hasunga amesema kuwa kufuatia kupitishwa kwa mtaala mpya unaojumuisha stadi na
programu za kilimo-hai katika vyuo vya mafunzo ya kilimo na vyuo vikuu kikiwemo
SUA, inatarajiwa idadi hiyo ikiongezeka mara dufu. Vyama vikuu vya ushirika –
KCU, KNCU na KDCU pamoja na makampuni kama Biore, Biosustain, Biolands na OLAM  wamewezesha nchi yetu kufikia mafanikio hayo.
 
Pia,
ametoa mwito kwa wadau wa kilimo-hai nchini kufanya kazi kwa karibu na Wizara na
Taasisi zake na Serikali yote kwa ujumla ili kwa pamoja kuwezesha upatikanaji
wa uhakika wa chakula na lishe na masoko utakao boresha maisha ya watanzania
walio wengi kwenye sekta ya kilimo.
 
Amesema
kuwa baadhi ya changamoto katika kuendeleza kilimo-hai nchini ni pamoja na
uhakiki (certification) wa mazao hayo kuwa ya kilimo hai, fedha kwa ajili ya
uwekezaji katika kilimohai kibiashara, kutoyafikia masoko maalumu (niche
market) hususani katika nchi za Ulaya kutokana na kutokidhi vigezo vya masoko
hayo na tishio la mabadiliko ya tabianchi ambayo ni fursa katika kuendelea
kilimohai nchini.
 
Waziri
Hasunga amewahakikishia wadau wote waliohudhuria katika mkutano huo kuwa Wizara
ya kilimo itaendelea kushirikiana nao kwa karibu hivyo wasisite kuwasilisha
mapendekezo yao wakati wowote ili Serikali iyashughulikie kwa maslahi ya
kuendeleza kilimo-hai nchini.
 
Kadhalika,
amewasihi wadau wote kupitia kongamano hilo, kujadili na kuzitafutia ufumbuzi
changamoto hizo ili kuweza kuongeza uzalishaji kupitia kilimo-hai.