Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akisisitiza jambo wakati
wa kikao baina yake na Ujumbe kutoka Benki ya NMB pamoja na Wataalam
kutoka Wizara ya Madini.
Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Serikali ya Benki ya NMB, Vicky Bishubo,
akieleza jambo wakati wa kikao baina ya Benki hiyo na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini. Wengine wanaofuatilia ni Watalaam kutoka Benki hiyo.
Wataalam kutoka Benki ya NMB wakifurahia jambo wakati wa kikao baina yao
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msajil (hayupo pichani)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila katika picha ya pamoja
na Ujumbe kutoka Benki ya NMB pamoja na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini,
Athony tarimo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini prof. Simon Msanjila akiongoza kikao baina ya
Ujumbe wa Benki ya NMB na Wizara ya Madini.
Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini Anthony Tarimo akifuatilia sambamba na
Mtaalam kutoka benki ya NMB Josephine Kulwa wakari wa kikao baina katibu
Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila na Ujumbe kutoka Benki ya NMB.
***************************************
Na Asteria Muhozya, Dodoma
Benki ya NMB imeshauriwa kutumia fursa za Kibiashara zilizopo
katika Sekta ya Madini zikiwalenga Wachimbaji Wadogo na wa
Kati wanaofanya shughuli hizo katika sekta husika ikiwemo
kujifunza namna biashara ya Madini inavyofanyika.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof.
Simon Msanjila wakati wa kikao baina yake na Ujumbe wa
Wataalam kutoka Benki hiyo ulioongozwa na Mkuu wa Idara ya
Mahusiano ya Serikali ya Benki hiyo, Vicky Bishubo. Kikao hicho
kimefanyika Novemba 25, 2019, jijini Dodoma.
Aidha, kauli ya Katibu Mkuu kwa benki hiyo inafuatia juhudi za
Serikali kupitia Wizara ya Madini zinazolenga katika kuwapatia
elimu Wachimbaji ikiwemo za kutunza kumbukumbu za uzalishaji,
kufanya tafiti ili kujua kiasi cha mashapo kupitia Taasisi ya Jiolojia
na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), na Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO), hayo yote yakilenga katika kuwawezesha wachimbaji
hao kukopesheka na Taasisi za Fedha.
Pia, Prof. Msanjila ameitaka benki hiyo kutumia fursa zilizopo
katika masoko ya Madini yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali
nchini ili kurahisisha biashara ya Madini na kutolea mfano wa
Soko la Madini Arusha kwamba benki hiyo haina huduma katika
soko hilo huku biashara ya Madini sokoni hapo ikifanyika kwa kiasi
kikubwa.
Aidha, Prof. Msanjila ameitoa wasiwasi benki hiyo kuwa, hivi sasa
biashara za Madini zinafanyika katika mfumo ulio wazi tofauti na
ilivyokuwa awali na kuongeza kwamba, “kuna biashara nyingi
kwenye sekta ya madini. Niwaambie hivi karibuni Serikali ya Qatar
itaanza kununua dhahabu moja kwa moja kutoka Geita.”
Katika hatua nyingine, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 35(j) ya
Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015-2020
kuhusu Kusimamia na kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za
uongezaji thamani madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo katika
Pato la Taifa, Prof. Msanjila ameishauri benki hiyo kuangalia
namna ya kufanya biashara katika tasnia ya ukataji wa madini,
akieleza kwamba, ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele na serikali ya kuhakikisha madini yanaongezwa
thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
“Sekta ya madini haijatumiwa vizuri na mabenki ninawakaribisha
kwenye sekta hii . Pale Arusha ndo mji pekee wa Ukataji Madini ya
Vito. Mwende mkaliangalie hili,” amesisitiza Prof. Msanjila.
Naye, Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Serikali ya Benki hiyo,
Vicky Bishubo amemshukuru Prof. Msanjila kwa kueleza fursa
zilizopo katika sekta husika na kueleza kwamba, benki hiyo
imeyachukua kwa uzito mkubwa yote yaliyoelezwa na iko tayari
kuyafanyia kazi.
“Tumejifunza namna sekta ya Madini inavyofanya kazi kuna
uwezekano wa sisi kuandaa mfumo wa kuwasaidia wachimbaji
wadogo,” ameeleza Bishubo.