*******************************
MRATIBU wa Program ya Kuendeleza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) Kitaifa, Emmanuel Msofe amezitaka halmashauri na vijiji vyenye misitu kwenda kujifunza uhifadhi na endelezaji misitu wilayani Handeni mkoani Tanga.
Msofe alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea Msitu wa Tarawe uliopo katika Tarafa cha Mazingira wilayani humo.
Alisema Msitu wa Tarawe umejaliwa vivutio vingi huku ukiendelea kuwa msitu asili kutokana wananchi kushirikiana na halmashauri kuutunza.
Msofe alisema FORVAC imeamua kushirikiana na vijiji ili kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu hali ambayo itaweza kuwanufaisha wananchi kiuchumi, kijamii na maendeleo.
Alisema FORVAC inatamani kuona halmashauri za wilaya na vijiji vyenye misitu kutembelea na kujifunza namna ya kuendeleza rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
“Program ya FORVAC inahakikisha rasilimali misitu inakuwa na mnyororo wa thamani kwa kugusa jamii ambayo inazungukwa na misitu hiyo, hivyo nitumie nafasi hii kuziomba halmashauri na vijiji vyenye rasilimali hiyo kuja kujifunza hapa Handeni,” alisema.