Mkurugenzi wa Mafunzo, Tafiti na Takwimu wa OSHA, Bw. Joshua Matiko, akiwasilisha mada kuhusu kampeni ya ‘Vision Zero’ kwa wanachama wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo wa mkoani Manyara.
Baadhi ya wanachama wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo ya mkoa wa Manyara wakifuatilia semina kuhusu utekelezaji wa kampeni ya ‘Vision Zero’ iliyotolewa na OSHA mjini Babati.
*************************************
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeitambulisha kampeni yake ya “Vision Zero” kwa waajiri wa mkoa wa Manyara na kuwahimiza kujiunga kwa hiari na mpango huo ambao una lengo kutokomeza ajali katika sehemu za kazi.
Akizungumza mara baada ya kutoa semina kuhusu utekelezaji wa kampeni hiyo kwa waajiri hao ambao ni wanachama wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo, Mkurugenzi wa Mafunzo, Tafiti na Takwimu wa OSHA, Bw. Joshua Matiko, amesema endapo waajiri wote nchini watauelewa na kuutekeleza ipasavyo mapango huo ni dhahiri kwamba hakutakuwa na ajali katika sehemu za kazi na hali ya usalama na afya itaimarika hapa nchini.
“Tunawashauri waajiri wote kujiunga kwa hiari yao katika kampeni hii kwani ina manufaa makubwa sana. Mkisha jiandikisha katika mpango huu tutawaomba mteue mwakilishi kutoka katika makampuni yenu ambaye tutamfundisha namna ya kutekeleza kampeni hii na yeye atakuwa na wajibu wa kwenda kuwafundisha wenzake katika eneo lenu la kazi,” alisema, Bw. Matiko.
Kwa upande wake, Juma Maneno, ambaye ni Kaimu Meneja wa OSHA, Kanda ya Kaskazini, amesema semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwakumbusha waajiri mambo ya msingi kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
“Tunashukuru tumepata mwitikio mkubwa sana hapa Manyara na wadau wetu
wameyapokea vizuri yale tuliyowaletea hivyo tunawaahidi kwamba mafunzo kama haya yatakuwa endelevu,” alieleza Juma Maneno.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wameeleza kufurahishwa kwao na kampeni ya “Vision Zero” pamoja na mafunzo mengine waliyoyapata katika semina hiyo.
Emmanuel Mgira, Mshauri wa Biashara TCCIA mkoa wa Manyara alisema: “Miongoni mwa majukumu yetu sisi kama TCCIA ni pamoja na kuwaunganisha wafanya biashara na mamlaka mbali mbali za serikali. Hivyo tumeona ni muhimu leo tukawaita OSHA ili waweze kuwaelekeza wanachama wetu mambo muhimu ya kuzingatia katika biashara zao hususani kwenye eneo la Usalama na Afya kwa wafanyakazi.”
“Tumefurahi leo OSHA wametupatia mafunzo mazuri sana na tumeweza kuelewa kwa kina juu ya shughuli wanazozifanya na namna wanavyozifanya. Hata hivyo tunawaomba waendelee kutoa mafunzo haya isiwe mwisho. Kuna wenzetu wengi huko vijijini hawafikiwi na luninga wala huduma za redio hivyo tunawaomba OSHA wafike hadi huko maeneo ya pembezoni kwaajili ya kusambaza elimu hii,” alisema Anna Ulomi, ambaye alishiriki semina
hiyo.
Dhana ya “Vision Zero” ilibuniwa na Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi za Jamii Duniani (ISSA) na dhana hiyo inatekelezwa na nchi mbali mbali duniani kwa namana fofauti kutegemeana na mazingira ya nchi husika.